Wanajeshi kunyogwa hadi kufa
Ni kwa mauaji ya mtoto wa Fundikira
Ndugu wa Marehemu wachekelea
Ndugu wa Marehemu wachekelea
Askari Magereza wakiwasindikiza washtakiwa wa kesi ya mauaji ya Swetu Fundikira.
Swetu Fundikira, alikuwa mtoto wa mwanasiasa maarufu nchimi, marehemu Chifu Abdallah Said Fundikira.
Kesi hiyo iliyovuta hisia ya wanaodaiwa
kuwa wanafamilia wa pande zote mbili tangu ianze kusikilizwa mahakamani
hapo Juni, mwaka huu, hukumu yake ilisomwa jana na Jaji Zainabu Miruke,
baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili.
Mamia ya watu walifurika katika ukumbi
namba moja wa mahakama hiyo mapema jana saa 2:30 asubuhi kwa ajili ya
kusikiliza hukumu hiyo.
Saa 4:28 asubuhi, Jaji Mruke aliingia kwenye ukumbi huo na kuanza kusoma hukumu hiyo huku utulivu ukiwa umetawala.
Jaji Mruke alisema washitakiwa wanatuhumiwa kwa kosa la mauaji ya makusudi kinyume cha sheria.
Alisema Oktoba 5, mwaka 2011, washtakiwa
walifikishwa mahakamani hapo na waliposomewa mashitaka yao na maelezo ya
awali, walikana isipokuwa majina yao na ajira zao.
Kutokana na washtakiwa kukana mashitaka
dhidi yao, upande wa Jamhuri uliita mashahidi sita, ambao walitoa
ushahidi dhidi ya tuhuma za mauaji hayo kuthibitisha mashitaka bila
kuacha shaka.
Jaji alisema pamoja na mashahidi hao,
upande wa mashitaka ulikuwa na jukumu la kuthibitisha mambo makuu manne
kama kweli Swetu amekufa, alikufa kifo ambacho siyo cha kawaida,
washtakiwa walihusika na kifo hicho na Mahakama ielezwe kama washtakiwa
waliua wakiwa na nia ovu au la.
Kwa mujibu wa Jaji Mruke, upande wa
Jamhuri ulipaswa kuithibitishia Mahakama jinsi nia ovu ilivyotumika
ikiwamo kueleza kama washtakiwa walitumia silaha, aina ya silaha
waliyotumia, nguvu iliyotumika ili kutimiza nia ovu, tabia ya washtakiwa
kabla na baada ya tukio na majeraha mangapi walimsababishia marehemu.
Alisema katika ushahidi na shahidi wa nne
ambaye ni daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu,
alithibitisha kwamba Fundikira alikufa kwa sababu ya majeraha
yaliyotokana na mkandamizo wa kitu chenye ncha kali.
“Pamoja na hayo, hakuna shahidi aliyesema
mahakamani hapa kwamba aliwaona washtakiwa wakimuua Swetu, lakini
mashahidi wa kwanza, wa pili na wa tatu walidai kwa nyakati tofauti kuwa
waliwakuta washtakiwa wakiwa na marehemu akiwa hai na mzima wa afya,”
alisema Jaji Mruke na kuongeza:
“Ushahidi wa Jamhuri uliotolewa mahakamani
hapa ni wa mazingira, washtakiwa walikutwa na marehemu akiwa mzima wa
afya na baadaye shahidi wa tano aliwakuta akiwa mikononi mwao
hajitambui, alikuwa mtupu kama alivyozaliwa na eneo ambalo siyo salama.”
Jaji alisema kuwa ushahidi wa mazingira
unatakiwa uwe kwenye mtiririko kama mnyororo ambao utatoa jibu moja,
mazingira yaelekeze kidole kwa washtakiwa na muingiliano wa ushahidi uwe
mmoja dhidi ya washtakiwa.
HUKUMU YA JAJI
“Katika kesi hii, ushahidi wa mazingira
unawanyooshea kidole washtakiwa moja kwa moja, wanahusika na mauaji
haya…kwa kuwa mashahidi wa Jamhuri bila kuacha shaka wamethibitisha
kuwaona washtakiwa wakiwa na marehemu mzima wa afya na baadaye wakiwa
naye eneo lingine hajitambui na amevuliwa nguo zote, Mahakama hii
inawatia washtakiwa wote hatiani,” alisema Jaji Mruke huku akipata
kikohozi mara kwa mara baada ya kueleza kuwa sauti yake haitakuwa nzuri
kwa sababu anasumbuliwa na mafua.
Mahakama ilimpa nafasi wakili wa utetezi, Kaloli Mluge, kuomba huruma ya Mahakama ili washtakiwa wapunguziwe adhabu.
Alidai kwa nyakati tofauti kwamba bado
umri wao ni mdogo, wanahitajika kwenye ujenzi wa taifa na wana familia
zinawategemea wakiwamo wazazi wao.
Jaji Mruke alisema kwa mujibu wa kifungu
cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, bila kuacha shaka, Mahakama imewatia
hatiani na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji hayo kama
walivyokuwa wanashtakiwa.
Januari 27, mwaka 2010, washtakiwa hao
walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu
Mkazi, Genivitus Dudu kwa usikilizwaji wa kesi wa awali.
Baada ya upelelezi kukamilika, kesi hiyo
ilihamishiwa katika Mahakama Kuu kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haikuwa na
mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Upande wa Jamhuri uliita mashahidi sita na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi watatu.
BAADA YA HUKUMU
Baada ya hukumu hiyo kusomwa kwenye viunga
vya mahakama hiyo, vilio vilitawala kutoka kwa wanaodaiwa kuwa ndugu wa
pande zote mbili na baadhi yao kupoteza fahamu.
Hata hivyo, wakili wa utetezi Mluge,
alisema hajaridhika na hukumu hiyo hivyo leo anatarajia kuwasilisha nia
ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani.
Washtakiwa walimuua kwa makusudi Swetu Januari 23, mwaka 2010, saa 7:30 usiku Kinondoni katika barabara ya Mwinjuma.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment