Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, alisema Tanzania imelaani waasi kuteka mji wa
Goma na kwamba ni jambo lisilokubalika wala kuvumilika tena.
Membe alisema kitendo cha waasi kuuteka
mji huo na kutangaza kutaka kuteka miji zaidi ukiwamo wa Bukavu ni jambo
la hatari na linalopaswa kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
Alisema msimamo wa Tanzania upo bayana
kwamba iko tayari kupeleka kikosi kimoja cha wanajeshi 800 na nchi
nyingine za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) zitachangia
majeshi mengine ili kufikia wanajeshi 4,000 wanaohitajika.
Hata hivyo, Membe alisema majeshi ya
Tanzania yataondoka nchini baada ya nchi nyingine kukubali kutoa idadi
nyingine ya wanajeshi wanaohitajika na pia kuafikiana namna ya kuvamia
nchi hiyo kukabiliana na waasi.
Alisema nchi za Sadc zipo tayari kupeleka
majeshi ya kuisaidia serikali ya DRC, lakini katika hali ya kushangaza
Umoja wa Mataifa (UN), umezizuia huku ukitazama waasi wakiteka miji na
kufanya uhalifu wa kibinadamu.
Waziri huyo alisema hali ya DRC
inasikitisha na inatisha, lakini UN imezuia wanajeshi kupelekwa nchini
humo kwa kisingizio kwamba kuna majeshi yanayolinda amani uko wakati
hayana nguvu kisheria za kupambana na waasi wala kupigana vita.
“Tunasikitishwa na wenzetu wa vikosi vya
UN kuendelea kuangalia tu hali ya usalama, lakini havina uwezo wa
kukabiliana na vita. Tulilalamika kwamba ingawa kuna majeshi ya UN,
lakini hayana uwezo wa kukabiliana na wapinzani. Wanachofanya ni
kuangalia tu wapinzani wako wangapi, wako wapi, wakimbizi wangapi
wamepatikana na wangapi hawana chakula, tunasema kwa utaratibu huu
hatufiki mbali,” alisema Membe.
Alisema dawa pekee ya kuinusuru DRC ni kwa
Sadc kupeleka jeshi nchini humo kwa ajili ya kulinda mipaka na
kuwalazimisha waasi waweke silaha chini ili utawala wa sheria uwepo
nchini au majeshi ya UN yaliyopo nchini humo kuruhusiwa kupambana na
waasi hao.
“Tanzania imekubali kujitolea kupeleka
kikosi kimoja Kongo na hata nchi nyingine za Sadc ziko tayari kufanya
hivyo hata kesho (leo) asubuhi,” alisema Membe.
Alisema kitendo cha waasi wakundi la M23
kuteka Goma kimesababisha wananchi wengi kukimbia makazi yao na wanawake
kubakwa na kutangaza kutaka kuuteka miji ya Bukavu na Kinshasa.
Alisema waasi kuachiwa kuteka miji
hususani wa Bukavu, Tanzania itaathiriwa vibaya na uhalifu huo kwa kuwa
wakimbizi watakimbilia nchini.
“Tumeomba na tunaendelea kuomba kwamba
Katibu Mkuu wa UN akipe nguvu kikosi chake kilichopo Goma na Kivu kibali
cha kukabiliana na waasi badala ya kuendelea kuangalia amani
ikivurugika DRC, kwamba UN wasikubali tena kuona watu wakidhalilika
katika nchi yao huku majeshi ya UN yakiangalia tu. Lakini tumeomba pia
sisi turuhusiwe kupeleka majeshi yetu yakapambane na waasi,” alisema
Membe.
VIONGOZI SADC KUKUTANA
Membe alisema leo na kesho, viongozi wakuu
wa Sadc watakutana jijini Kampala, Uganda kujadili namna ya kuinusuru
DRC hata kama UN itaendelea kushikilia msimamo wake, viongozi hao
watatoa uamuzi mgumu.
Kuhusu tuhuma kwamba Serikali ya Rwanda
pamoja na Uganda zinawasaidia waasi, Membe alisema inasikitisha viongozi
wa nchi hizo kutokaa na kumaliza tofauti zao na katika mkutano wa leo
na kesho, Rais Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda,
watahudhuria.
Waasi wa M23 waliibuka Aprili mwaka huu
kwa madai ya kupinga maazimio ya Machi 23 mwaka 2009, yaliyofikiwa
wakati Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na aliyekuwa Rais wa
Nigeria, Olusegun Obasanjo, walipokuwa wakisuluhisha mgogoro wa DRC.
Vitendo vya wapiganaji hao wa M 23 vimezua
wasi wasi wa kuzuka upya kwa mapigano nchini DRC, ambako takriban watu
milioni tano waliauawa kufuatia mapigano yaliyoanza mwaka wa 1997 na
kumalizika mwaka 2003.
Jumanne wiki hii, waasi hao waliuteka Goma uliopo Mashariki mwa DRC unaoelezwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini.
Hii ni mara ya kwanza kwa waasi kufanikiwa kuteka Goma tangu kumalizika kwa mapigano mwaka wa 2003.
Kumekuwa na taarifa za Serikali ya Rwanda kuhusika kuwasaidia waasi hao, lakini imekuwa ikikanusha.
Baraza la Usalama la UN limelaani kutekwa
kwa mji huo na mapigano yameelezwa kuwa mabaya zaidi tangu waasi
walipoanzisha vita Julai mwaka huu.
Tayari Rais wa DRC, Joseph Kabila, ambaye
aliapa kuulinda Goma, amekubali kuanzisha mazungumzo na waasi hao. Juzi
wapiganaji hao wa M23 waliuteka mji wa Sake, ulioko takriban kilomita
27, kutoka Goma.
Ripoti zinasema wapiganaji hao sasa wanajiandaa kuelekea eneo la Kusini hadi Bukavu, takriban kilomita 230 kutoka Goma.
Wakati huo huo; Membe amesema taarifa ya
kikao cha kamati ya mambo ya nje kuhusu suala la Malawi imekabidhiwa kwa
Rais Jakaya Kikwete na kwamba lengo ni kwa Rais Kikwete kukutana na
Rais wa Malawi, Joyce Banda, ili kutafuta mwafaka.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment