Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa
Habari zilizosambaa kupitia simu za
mikononi na watu mbalimbali waliokuwa wakipiga simu chumba cha habari,
zilidai kuwa Dk Slaa ambaye alikuwa safarini katika ziara yake ya kikazi
amepata ajali ya gari maeneo ya Dodoma na Morogoro na kufariki dunia.
Habari hizo hata hivyo zilikanushwa na Dk. Slaa mwenyewe baada ya kupigiwa simu yake ya mkononi.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi, Dk.
Slaa alisema anamshukuru Mungu kuwa hao wanaomzushia kifo wanazidi
kumuongezea maisha na kumpa nguvu na kuendelea na kazi zake.
“Hizo ni propaganda za watu wasionitakia
mema, hivi ninavyoongea na wewe niko katika kijiji cha Nkwenda, Wilaya
mpya ya Kyelwa, huku Bukoba ndio nimetoka kuteremka kwenye jukwaa
kuongea na wananchi,” alisema Dk. Slaa na kuongeza “Mimi ni mzima kabisa
na nikitoka hapa nakwenda kwenye mkutano mwingine.”
Alisema hiyo si mara ya kwanza yeye
kuzushiwa kifo, lakini anamshukuru Mungu kuwa wabaya wake wanavyozidi
kumzushia habari mbaya wanaendelea kumuongezea siku za kuishi.
Dk. Slaa alisema anaamini watu wanaozusha
habari hizo wana nia mbaya ya kumdhoofisha kisiasa lakini kwa uwezo wa
Mungu ataendelea kupigania haki za wananchi.
Akidhihirisha kuwa yu mzima wa afya, Dk.
Slaa alisema anaendelea na kazi zake za chama na kwamba akitoka kwenye
wilaya hiyo mpya anaekelekea kwenye wilaya nyingine kwa kazi yake ya
kueneza sera ya chama chake.
Dk Slaa pia alikiri kupokea simu kutoka
kwa watu mbalimbali waliokuwa wakiulizia hali yake baada ya kuenea kwa
habari za kuzushiwa kifo.
“Nashukuru kuwa watu wananipenda maana
baada tu ya kupata habari hizo walikuwa wakinitafuta kwenye simu yangu
kujua ukweli,” alisema.
Hii ni mara ya pili kwa Dk. Slaa kuzushiwa kifo, mara ya kwanza aliwahi kuzushiwa kuanguka bafuni na kupoteza maisha.
Tabia hii ya watu hasa maarufu kuzushiwa
taarifa za vifo imekuwa ni mtindo kwa baadhi ya watu na kusababisha
usumbufu mkubwa kwa familia, ndugu na jamaa za watu hao.
Watu wengine wanaolengwa na habari hizo za
kizushi ni pamoja na wasanii wenye majina makubwa na hivi karibuni
msanii wa siku nyingi maarufu kama Bi Kidude aliwahi kuzushiwa kifo.
SOURCE:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment