Na Beatrice Shayo
Mamlaka
ya Mawasiliano nchini (TCRA), imesema haitaongeza muda wa kujiunga na
mfumo wa digitali na ifikapo Desemba 31, mwaka huu itakuwa mwisho wa
kutumia teknolojia ya zamani ya analogia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam, Meneja wa Mawasiliano TCRA, Innocent Mungy, katika
semina ya wadau wa Manispaa ya Temeke juu ya haki na wajibu wa
watumiaji wa huduma za mawasiliano, alisema wananchi wanatakiwa
kuzingatia muda uliowekwa.
Alisema ikifika Desemba 31 mwaka huu,
kama kutakuwa na mtu ambaye hajajiunga na mfumo wa digitali hataweza
kuona matangazo wala kurusha, hivyo ni muhimu watu kutafuta ving'amuzi
mapema.
Mungy alisema mtu yeyote ambaye atanunua
king'amuzi hataingia gharama za kulipia kwa mwezi na kwamba atakuwa
akiona matangazo ya televisheni za ndani bure lakini akitaka kuona
matangazo ya vituo vya kimataifa kama CNN, BBC na KBC atalipia.
Hata hivyo, alisema baadhi ya wananchi
hawajawa na uelewa kuhusu mfumo huo mpya na kudhani wanatakiwa kununua
televisheni mpya.
Alisema kinachotakiwa ni kununua king'amuzi kutoka kampuni za Star Times au Agape lakini televisheni zitakazotumika ni zilezile.
Alisema tayari kampuni hizo zimeshajulishwa kuwa zitatakiwa kuonyesha vipindi vya nchini bure.
Akizungumzia suala la kuwepo kwa simu feki
nchini, Mungy alisema wanajipanga kwa kushirikiana na mamlaka nyingine
katika kuzuia tatizo hilo.
Alisema kwa sasa wanachokifanya ni kutoa mafunzo kwa wananchi hasa katika maeneo ya vijijini kuacha kununua simu feki.
Mungy alisema endapo wakizuia simu hizo
zisitumike kwa sasa wananchi wengi wataathirika zaidi katika zoezi hilo,
hivyo wanalifanyia kazi na watatoa taarifa ya kusitishwa kwa utumiaji
wa simu feki ili watu wasiathirike.
Kwa upande wake mjumbe ambaye alikuwa
akiwakilisha chama cha wazee, Bregadia Jenerali Mstaafu, Francis Mbeuna,
alisema mafunzo ambayo yanatolewa na TCRA yatawasaidia kujua haki zao
ya msingi.
Alisema anaunga mkono suala la kuingia
kwenye mfumo wa digitali na kwamba inaonyesha kuwa Tanzania inakwenda na
wakati kama nchi zingine.
Naye Diwani wa Viti maalum Temeke, Mariamu
Mtevu, alisema kuwa serikali iangalie namna ya kuwapunguzia ving'amuzi
hivyo ili kila mmoja aweze kuvinunua kwani gharama ni kubwa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment