Wednesday, November 21, 2012

Di Matteo afutwa kazi

Roberto Di Matteo amefutwa kazi na klabu ya Chelsea, baada ya kuwa meneja kwa kipindi cha miezi minane.
Di Matteo aliiwezesha Chelsea kuwa mshindi wa klabu bingwa barani Ulaya, na vile vile kupata Kombe la FA msimu uliopita, na mwezi Juni, alitia saini mkataba wa miaka miwli.
Lakini kufuatia Chelsea kuzabwa magoli 3-0 na Juventus usiku wa Jumanne, inaelekea timu hiyo itakuwa na kibarua kigumu sana cha kufanikiwa kuendelea katika michuano ya klabu bingwa, na kwa hiyo wasimamizi wa klabu wameonelea ni vyema kumtimua kutoka Stamford Bridge.
Kulingana na taarifa katika mtandao wa Chelsea, "klabu kitatoa taarifa kamili hivi karibuni kuhusiana na meneja wa timu".
Roman Abramovich, tajiri anayemiliki klabu ya Chelsea, sasa atakuwa anamtafuta meneja wa tisa, tangu kumiliki klabu mwaka 2003, na kwa muda mrefu, inaaminika amekuwa akizitamani sana huduma za aliyekuwa meneja wa Barcelona ya Uhispania, Pep Guardiola.
Lakini vile vile amewasiliana na aliyekuwa kocha wa Liverpool ya Uingereza, Rafael Benitez, na kuna uwezekano huenda akashikilia hatamu kwa muda mfupi.
Abramovich, raia wa Urusi, tayari alikuwa amewasiliana na Benitez hata kabla ya Chelsea kushindwa nchini Italia.


chanzo BBC swahili

No comments: