Friday, November 23, 2012

Spika wa Bunge asitokane na chama`

Na Mwandishi wetu

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamesema Spika wa Bunge asitokane na chama cha siasa ili kuepusha upendeleo bungeni.
Wakitoa maoni ya Katiba Kpya katika viwanja vya Shule ya msingi Tabata Kimanga wilayani, Ilala jana, walisema Spika akitokana na chama cha siasa anakuwa na nafasi ya kukipendelea chama chake.
Marko Palanjo, alisema Spika achaguliwe kutoka katika taasisi au mtu binafsi ili kuwe na uhuru na usawa bungeni.
“Hili suala la Spika kutoka katika chama linamfanya kuwapendelea waliomchagua,” alisema John Mchimbi.
Salum Abdalah, alisema kuwa Spika ataendelea kutokana na chama kilicho na idadi kubwa ya wabunge hivyo kukinyima haki chama kisicho na idadi kubwa ya wabunge.
Aidha, baadhi ya wananchi walipendekeza kwamba mtu anayetaka kugombea ubunge awe na elimu ya shahada ya kwanza ili kuondokana na tatizo la kuongozwa na viongozi wasio na sifa na elimu ya kutosha.
Godfrey Kalokola, alisema kwa sasa wabunge wamekuwa wakichaguliwa na kuongezwa mishahara bila ya kuwa na sifa na kikomo cha elimu, jambo linalopelekea ubunge kuwa kama sehemu ya kimbilio kwa watu wasio na sifa.
Wanachi hao pia walitaka sheria ya kunyongwa kifutwe ili kuepusha mlundikano wa wa fungwa walioko magereza wasio na kazi za kufanya wakisubiri kunyongwa.
“Sheria hii ifutwe ili kumuondolea Rais kigugumizi cha kutokusaini kunyongwa kwa wafungwa, kwa sababu yeye mwenyewe anakwepa kuua kutokana na mamlaka hayo kuwa nayo yeye peke yake,” alisema Makame Mpate.
CHANZO: NIPASHE

No comments: