Thursday, November 22, 2012

Nacte yasema Agape haina sifa za kutoa Stashahada

Na Mwandishi wetu

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) limesema kuwa Chuo Cha Agape hakina Ithibati ya kukiwezesha kutoa mafunzo yoyote ya ngazi ya Stashahada, hivyo hakiwatambui wanafunzi zaidi ya 33 wa ngazi hiyo waliohitimu masomo yao chuoni hapo.
Akizungumza na NIPASHE j jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Primus Nkwera, alisema kuwa, chuo hicho kilipata usajili wa awali kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ngazi ya cheti, wakati kikiendelea kufuata taratibu mbalimbali kilichopewa na baraza hilo ili kiwe na sifa stahiki.
Dk. Nkwera alisema kuwa mbali na chuo hicho kusajiliwa mwaka 2010, na kupewa maelekezo ya kufuata ili kukamilisha taratibu za kupata sifa stahiki, lakini hakikufanya hivyo badala yake kiliamua kutoa mafunzo ya ngazi ya Stashahada kwa makubaliano na Chuo Cha Taifa Cha Biashara (CBE), jambo ambalo halikubaliki kisheria.
Alisema kuwa alipata taarifa za kuwapo kwa makubaliano kati ya vyuo hivyo viwili, na alipoamua kufuatilia aligundua kuwa mkataba walioingia haupo kisheria kwani CBE haina uwezo wala mamlaka ya kusajili chuo kingine.
“Ni kweli kuna taarifa za kuwapo kwa mkataba wa makubaliano kati ya vyuo hivyo, niliukabidhi mkataba huo kwa wataalam wa sheria ambao waliniambia kuwa mkataba huo ni batili,” alisema Dk.Nkwera.
Aidha, Dk. Nkwera alisema atauandikia uongozi wa CBE ili kuuonya kutokana na kukiuka utaratibu, na wakati huo huo akisuburi taarifa ya wakaguzi wa baraza hilo waliokitembelea chuo hicho hivi karibuni ili achukue hatua.
Akizungumzia malalamiko ya wanafunzi hao, Dk. Nkwera, alisema kuwa ni vyema wakawasiliana na baraza hilo ili kuangalia nini cha kufanya kuwawezesha watambuliwe na baraza hilo na kuendelea na masono ya juu.
John Nzena, mwanafunzi aliyehitimu masomo yake chuoni hapo mwaka huu, aliiambia NIPASHE kuwa alijiunga na chuo hicho mwaka 2010 kwa kozi ya Stashahada ya Ugavi, lakini alipomaliza mwaka huu na kuanza taratibu za kujiunga na elimu ya ngazi ya juu kwenye vyuo vingine, aliambiwa kuwa chuo alichotoka hakitambuliki.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Dk. Leonard Mbilinyi, alisema kuwa amepata malalamiko ya wanafunzi hao kuhusiana na kukataliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, na kusema anashangwazwa na kuwepo kwa taarifa ya kwamba hakuna mkataba wa makubaliano yaliyofanywa kati ya chuo chake na CBE.
Dk. Mbilinyi alisisitiza kwamba mkataba huo ni halali kwani ulishirikisha pande zote mbili, na kwamba nyaraka zote anazo, kinachofanyika sasa ni mazungumzo kati yake yeye, CBE na Nacte ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: