Wednesday, December 5, 2012

Serikali kuzungumza na wapiganaji Mali

Wapiganaji wa Tuareg wameteka kaskazini mwa Mali
Serikali ya Mali imekubali kushiriki katika mazungumzo na wapiganaji wa Tuareg pamoja na waasi wenye itikadi kali za dini ya kiislamu katika jitihada za kuiunganisha upya nchi hiyo.
Baada ya kukutana na maafisa wa serikali , makundi ya upinzani yaliahidi kuheshimu hadhi ya kieneo ya Mali na kupinga ugaidi.
Wapiganaji wa Tuareg na wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya kiislamu walidhibiti sehemu kubwa za Kaskazini mwa Mali baada ya mapinduzi yaliyofanyika mnamo mwezi Machi.
Mazungumzo hayo yaliyopendekezwa hayatojumuisha makundi mengine mawili yaliyojihami ambayo serikali inasema yanajumuisha wapiganaji wa nje wa Al Qaeda katika eneo la Magharibi mwa Afrika na MUJAO.
Serikali za kikanda hivi karibuni ziliidhinisha mipango ya kutuma zaidi ya wanajeshi elfu tatu Kaskazini mwa Mali punde tu watakapo pata idhini ya Umoja wa mataifa.

No comments: