Na Dege Maso
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameendelea kuwa mwiba mkali kwa kupiga marufuku usafiri wa daraja la kwanza kwa watendaji wakuu wanaokwenda nje ya nchi na kutangaza kuchukua hatua kali kwa watakaokiuka agizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Jijini hapa, Dk. Mwakyembe alisema agizo hilo linawahusu watendaji wakuu
wa mashirika yote yaliyopo ndani ya Wizara ya Uchukuzi.
Alisema lengo la marufuku kwa watendaji
hao kutumia usafiri wa daraja la kwanza ni kuzuia ufisadi na matumizi
mabaya ya kodi za wananchi ambao ni walalahoi.
“Mimi Waziri natumia usafiri wa daraja la
pili kwenda nje ya nchi, lakini watendaji wakuu wanatumia daraja la
kwanza…jambo hili halipendezi na wenzetu wa nchi nyingine
wanatushangaa,” alisema.
Dk. Mwakyembe alionya kwamba yeyote
atakayebainika kwenda kinyume na agizo hilo atachukuliwa hatua ikiwemo
kukatwa fedha za usafiri katika mafao yake.
Waziri Mwakyembe yupo Jijini hapa kwa ajili ya kukutana na bodi mpya ya wakurugenzi na kupanga mikakati ya utendaji.
Pia alitangaza mkakati wa kuzuia usajiri
wa vyombo vya majini vyenye umri wa zaidi ya miaka 15 kwa lengo la
kudhibiti ajali za majini.
Alisema mkakati mwingine ni kuhakikisha
kila chombo chenye sifa ya kutoa huduma za usafiri wa majini kinakuwa na
vifaa vya kutosha vya uokoaji na kupakia kwa mujibu wa uwezo wa chombo
husika na kwamba kila abiria ataruhusiwa kupanda ndani ya chombo hicho
kwa kutumia kitambulisho cha uraia na si vinginevyo.
Kwa upande mwingine, Dk. Mwakyembe alisema
serikali ya Tanzania pamoja na ya Denmark imeanza mchakato wa kupata
meli mpya kubwa ambayo itakuwa suluhu la tatizo la usafiri wa majini
pamoja na kuangalia uwezekano wa kusimamisha meli za zamani ikiwemo ya
MV. Liemba ambayo inakaribia takriban miaka 100 sasa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment