Thursday, November 22, 2012

MFUNGWA KUKUTWA URAIANI NA SMG: Polisi, Magereza wakinzana kwa kauli


Sakata la mfungwa aliyekutwa uraiani akiwa na bunduki na risasi, limeingia katika hatua mpya baada ya Jeshi la Polisi na Magereza kutoa kauli zinazokinzana.
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu limeendelea kuthibitisha kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa nyumbani kwake Novemba 16, mwaka huu akiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), risasi 31 na magazini tatu, Masanja Maguzu (42), ni mfungwa ambaye hajamaliza kutumikia kifungo cha miaka 15 jela na kuwa alitoka gerezani katika mazingira ya kutatanisha.
Wakati Jeshi la polisi likisisitiza hivyo, Jeshi la Magereza limetoa taarifa inayoeleza kuwa mtu huyo alishamaliza kifungo.
Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Salum Msangi, amekanusha madai ya Jeshi la Magereza kwamba mfungwa huyo alishamaliza kutumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka mitano jela na kwamba hata kama alikuwa akitumikia adhabu ya miaka mitano muda huo bado haujatimia.
Kamanda huyo alifafanua jana kuwa hata kama kuna tetesi za mfungwa huyo kuachiwa kwa msamaha wa Rais, makosa yaliyompeleka gerezani kwa mujibu wa Sheria ya Msamaha hayana msamaha.
Alisema mfungwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela mwaka 2010 baada ya yeye na mwenzake, Japhet Sylivester, kupatikana na hatia ya kukamatwa na SMG, risasi 622 na nyara za serikali (nyama ya nyati) akiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa).
Kamanda Msangi aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu kuwa leo atatoa taarifa kamili ya jinsi mfungwa huyo alivyotoka gerezani baada ya Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kubaini ukweli wa mazingira yaliyosababisha kuwa uraiani.
Alifafanua kuwa wafungwa hao walikuwa wakiitumia bunduki hiyo kufanyia vitendo vya uhalifu ukiwamo ujambazi na ujangili na siku hiyo walikamatwa nayo ndani ya hifadhi hiyo na risasi 74 na baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi na wa wanyamapori aliwapeleka nyumbani kwake kuwaonyesha alipokuwa ameficha nyingine 548.
Alidai kuwa wafungwa hao walikamatwa katika msako wa pamoja wa kukabiliana na vitendo vya uhalifu na kukabiliana na ujangili uliokuwa ukiendeshwa kwa pamoja kati ya askari wa Jeshi la Polisi na Wanyamapori mkoani Shinyanga kwa wakati huo.
Alisema baada ya kufunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Shinyanga, watuhumiwa hao walipatikana na hatia na hivyo kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 15 jela kila mmoja.
“Kesho (leo), nitatoa picha kamili ya jinsi mfungwa huyo alivyotoroka gerezani na kumuacha mwenzake waliyehukumiwa naye kifungo, hii ni baada ya kufanya uchunguzi wetu wa kina na kumhoji mfungwa mwenyewe na kubaini mambo kadha wa kadha yaliyosababisha yeye kuwa uraiani na kuendelea kufanya vitendo vya uhalifu na ujangili kwa kutumia silaha za kivita,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, wafungwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi ambayo ni kupatikana na bunduki, risasi, nyara za serikali na kuingia na kuwinda ndani ya hifadhi bila kibali na baada ya kupatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda gerezani, hayawezi kutolewa msamaha.
“Watuhumiwa hawa walipatikana na makosa ya kupatikana na bunduki ya kivita, kupatikana na risasi, kupatikana na nyara za serikali na kuingia kuwinda ndani ya hifadhi na kuwinda bila kibali nyume cha sheria makosa yote haya yanaangukia kwenye makosa ya uhujumu uchumi ambayo hayana msamaha kisheria,” aliongeza.
Alisema siku 10 kabla ya kumkamata mfungwa huyo akiwa uraiani na SMG hiyo, risasi 31 na magazini tatu, moja hutumika katika bunduki aina ya Uzi gun ya Kiisraeli, jeshi hilo lilikuwa limemkamata mke wake, Holo Mabuga (30), akiwa na bunduki ya kivita aina ya G3, risasi zake 36 pamoja na risasi nyingine zinazotumika kwenye bunduki aina ya SMG inayodaiwa pia kutumika katika matukio mbalimbali ya kihalifu na ujangili katika Senapa na Pori la Akiba la Maswa.
TAARIFA YA MAGEREZA
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Kaimu Kamishna wa Magereza, Deonice Chamulesile, ilisema Maguzu alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano, lakini Aprili 26, mwaka huu alikuwa ameachiliwa.
“Mfungwa aliyekuwa na Namba 250/2010, Masanja Maguzu, alipokelewa Gereza la Wilaya ya Shinyanga tarehe 3 Novemba, 2010 baada ya kuhukumiwa na Mahakama ya wilaya hiyo kwa makosa mbalimbali ya uhujumu uchumi,” alisema.
Aliongeza: “Alianza kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani kuanzia Novemba 3, 2010 na kufikia Aprili 26, 2012 aliachiliwa baada ya kutimiza masharti ya kifungo na kutoka gerezani kwa mujibu wa sheria, hivyo ifahamike kwamba hakutoka katika mazingira ya utata kama ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari.”
Taarifa hiyo iliyataja makosa aliyohukumiwa kuwa ni kuingia kinyume cha sheria katika hifadhi, kuwinda kunyume cha sheria na kumiliki kinyume cha sheria nyara za serikali.
Taarifa hiyo ya Chamulesile ilieleza kuwa katika kosa la kwanza, Maguzu alihukumiwa miaka miwili jela, kosa la pili miaka mitano jela na la tatu miaka mitano jela.
Alisema hukumu iliyotolewa iliamuru adhabu hizo zitumikiwe kwa pamoja kwa kufungwa miaka mitano jela.
CHANZO: NIPASHE

No comments: