Monday, November 26, 2012

Anayedaiwa kufufuka apelekwa polisi

Siku chache baada ya sakata la mwanamke anayedaiwa kufa na kufufukana, kisha baadaye kuingia nyumbani kwake usiku akiwa mtupu, limechukua sura mpya baada ya mwanamke huyo kuchukuliwa na mkuu wa wilaya ya Busega na kumpeleka polisi.
Mkuu wa wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya, alimchukua mwanamke huyo juzi na kumpeleka makao makuu ya polisi katika mkoa wa Simiyu kwa usalama wake.
“Nimemchukua mwanamke huyo na kumpeleka polisi kwa ajili ya usalama wake na kwa uchunguzi zaidi juu ya kisa hicho...pia mwanamke anayetuhumiwa kuwa mchawi alichukuliwa na polisi kwa ajili ya usalama wake sababu wananchi wenye hasira walitaka kumshambulia,” alisema Mzindakaya.
Mwili wa marehemu huyo ulizikwa saa 12 jioni katika mji wa mwanamke anayedaiwa kumuua mwanamke huyo Ngulima Kilinga (30), mkazi wa kitongoji cha Mwabulugu, kijiji cha Lamadi wilayani Busega.
Awali wananchi walikuwa wamekataa kuuzika mwili huo, kwa madai kuwa ni kitu kingine, ambapo mkuu huyo wa wilaya aliingilia kati na kuwashawishi hao kuachana na imani za kishirikina.
Kabla ya kumchukua mwanamke huyo pia mkuu huyo wa wilaya aliwahutubia wananchi, akiwaasa waachane na mambo ya imani za kishirikina na kusisitiza kuwa huyo aliyekufa ndiye mhusika na kwamba hakuna mtu aliyefufuka.
Alisema kuwa mwili wa mwanamke huyo ulibadilika na kuwa kama sura ya mzee kutokana na kukaa kwa kipindi kirefu bila kuwekwa kwenye jokofu, hali iliyosababisha tumbo kuvimba na kutaka kupasuka.
“Nimewataka wananchi waachane na imani hizo za ushirikina mimi ninaamini kwamba huyo mwanamke amekufa na wala hajafufuka kama inavyodaiwa na watu wakiwemo ndugu zake...mwili wa marehemu umebadilika kwa sababu haukuwekwa kwenye barafu,” alisema.
Kamanda wa polisi katika mkoa wa Simiyu, Salum Msangi, alikiri mwanamke huyo kufikishwa polisi.
Msangi alisema kuwa baada ya uchunguzi wa kina kufanyika, imebainika kuwa mwanamke huyo anayedaiwa kuwa ndiye aliyefufuka, ambaye mwili wake ulikuwa katika hospitali ya Mkula, si kweli kwani anaonekana kuwa ana upungufu wa akili.
Alisema kuwa mwanamke huyo ametambuliwa kwa jina la Kundi Balekele (30), mkazi wa kijiji cha Mwasuguya wilayani Bariadi.
Kamanda Msangi alisema kuwa mwanamke huyo alipotea nyumbani kwao kwa muda mrefu na kwamba huenda aliingia kwenye nyumba ya marehemu huyo, katika kitongoji cha Mwabulugu kwa bahati mbaya tu.
“Huyo mwanamke amekuwa akipotea mara kwa mara nyumbani kwao na amepotea kwa muda mrefu, na pale nyumbani aliingia kwa bahati mbaya maana ana upungufu wa akili,” alisema Msangi.
Alisema kuwa jana ndugu zake walifika kituoni hapo na kumchukua mwanamke huyo na kumpeleka kijijini kwao.
Aidha alifafanua kuwa kutokana na mwanamke huyo kuingia kwenye nyumba hiyo usiku akiwa mtupu, na kuanza kuvaa nguo za marehemu na kuangalia picha zake kwenye albamu, ikiwa ni pamoja na kuita majina ya watoto wa marehemu na kisha kulala kitandani, ndiyo sababu ndugu zake waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walidhani kuwa ndiye ndugu yao kwani hata umbo la mwili wake ulifafanana na marehemu.
Alisema kuwa kwa kuwa mwanamke huyo ana upungufu wa akili aliingia kwenye nyumba ya marehemu kwa bahati mbaya akiwa mtupu, na hivyo kuwashangaza waliokuwa ndani ya nyumba hiyo na kudhania kuwa ndugu yao amefufuka, kutokana na matendo aliyokuwa anafanya akiwa ndani ya nyumba hiyo.
Kwa upande wao ndugu wa marehemu akiwemo mama yake mzazi, Mwashi Myeya, alisema kuwa mwanamke aliyechukuliwa na mkuu wa wilaya ndiye mtoto wake kwani ana alama usoni ambayo alikuwa nayo kuanzia utotoni na kwamba hayo ni mazingara yamefanyika.
“Siwezi kumsahau mwanangu nimemuona anayo alama kwenye sehemu ya pua na hiyo alama ni kutoka utotoni alikuwa nayo,” alisema Myeya.
Wananchi hao walisema kuwa mwili wa marehemu waliouzika ni kitu kingine na ndio maana waliamua kuuzika kwenye mji wa mtuhumiwa wa uchawi, ambaye pia alitoroshwa na polisi kwa ajili ya usalama wake.
Aidha, wanadugu hao walisema kuwa iwapo mwanamke huyo asingetoroshwa na polisi, huenda angefanya dawa za kumtengeneza na kurudia hali yake.
Hata hivyo kabla ya mkuu wa wilaya kumchukua mwanamke huyo, aliletwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya kumtengeneza ili arudie hali yake, ambapo alidai apewe kiasi cha Sh. milioni 2.5 ambapo wananchi walianza kuchanga lakini pia hazikutimia.
Habari zinasema kuwa baada ya mkuu wa wilaya kufika katika eneo la tukio mganga huyo alitoweka katika eneo hilo katika mazingira ya kutatanisha na kutokomea kusiko julikana.
Imeelezwa kuwa mwanamke huyo alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Mkula inayomilikiwa na kanisa la AIC, ambapo mwili wake ulihifadhiwa chumba cha maiti.
Mashuhuda walisema kuwa saa 7 usiku mwanamke mmoja aliyekuwa mtupu alingia ndani ya nyumba ya marehemu na kuanza kuita watoto wake, ikiwa ni pamoja na kuvaa nguo za marehemu, ambapo ndugu zake walidhani kuwa amefufuka.
CHANZO: NIPASHE

No comments: