Wednesday, July 17, 2013

SIMANZI FAMILIA ZA ASKARI JWTZ

Vilio na simanzi vimetawala katika baadhi ya familia za askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao waliuwawa katika eneo la Darfur, Sudan ambako wanashiriki katika ulinzi wa amani.
Mamia ya waombolezaji walionekana katika makazi ya familia za marehemu; Songea mkoani Ruvuma na Nachigwea mkoani Lindi ambako ziko kambi ambazo baadhi ya askari hao walikuwa wakifanya kazi.
Imefahamika kuwa wanajeshi waliouwawa Jumamosi iliyopita wanatoka katika vikosi vya, 42KJ Chabruma, Songea,  44KJ Mbeya, 36KJ Msangani, 92KJ Ngerengere, 94KJ cha
Mwenge, Dar es Salaam, 41KJ Nachingwea na Makao Makuu ya JWTZ- Upanga, Dar es Salaam.
Jana gazeti hili lilibaini kuwapo kwa maombolezo katika baadhi ya familia za wanajeshi hao baada ya kupokea taarifa za vifo vyao kutoka JWTZ. Hata hivyo bado majina ya waliofariki hayajawekwa hadharani.
Msemaji Mkuu wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe juzi aligoma kutaja majina hayo akisema kuwa majina hayo hayajatolewa rasmi na kwamba familia za marehemu zilikuwa hazijajulishwa.
“Hayo majina yanayotajwa kwenye mitandao ni ya uongo. Kwa sasa mimi sijaletewa majina na utaratibu uliopo ni hadi ‘next of kin’ (ndugu) wao wajulishwe kwanza,” alisema Kanali Mgawe.
Hata hivyo kupitia katika maeneo ilikokuwa misiba hiyo jana, gazeti hili lilifanikiwa kufahamu majina ya baadhi yao, ambayo yanafanana na yale yaliyotangazwa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na baadhi ya magazeti.
Katika Kambi ya Chabruma, Songea mkoani Ruvuma kulikuwa na umati wa waombolezaji nyumbani kwa mmoja wa wapiganaji hao, Koplo Oswald Chaula ambaye alikuwa katika Kikosi cha Mizinga Chabruma na ndugu zake walikiri kupokea taarifa za msiba huo.
Hali kama hiyo ilikuwa nyumbani kwa Koplo Mohamed Chukilizo katika Kambi ya Majimaji, Nachingwea ambako baadhi ya ndugu na jamaa za zake wakiwamo mkewe na baba mkwe wake walikutana jana jioni kujadiliana kuhusu msiba.
Mwananchi pia lilishuhudia waombolezaji wakiwa wamekusanyika eneo la Mjimwema, Songea Mkoani Ruvuma ambako ni nyumbani kwa Komandoo Rodney Ndunguru aliyetoka kikosi cha 92KJ Ngerengere, Morogoro, baada ya kupokea taarifa za msiba huo. 
Vilio, Simanzi
Katika kambi ya Chabruma, mke wa marehemu Koplo Oswald aliyejitambulisha kwa jina la Maria alikuwa akilia kwa simanzi baada ya kupata taarifa kuwa miongoni mwa waliofariki ni baba watoto wake
“Ninamuomba Mungu ampumzishe mume wangu...nimekosa nini jamani, mume wangu kaondoka...alikuwa tegemeo langu. Sijui kama wanangu watasoma, dunia imenigeuka... imekuwa ghafla mno, Chau kaondoka bado nampenda,” alisikika akisema Maria huku akiwa amewakumbatia wanawawe. Ndugu na jamaa walikuwa wakimfariji.
Maria anatarajiwa kuondoka Songea leo kwenda katika kijiji cha Kilolo, mkoani Iringa kusubiri mwili wa mume wake ambaye atazikwa huko. Chaula ameacha watoto wanne, mmoja akiwa na umri wa miezi minne.
Katika eneo la Mjimwema mama wa marehemu Ndunguru, Lucy Ndunguru aliyekuwa akilia muda wote, alisema: “Mwanangu Rodney kaniacha...nilikuwa namtegemea, alikuwa ananitunza na mimi ni mjane sasa kaniacha...ee Mungu nimekosa nini mimi....”
Sauti yake ya mitetemo na kwikwi za simanzi viliwafanya baadhi ya waombolezaji nao kujikuta wakibubujikwa na machozi, huku kukiwa na taarifa kwamba wanapanga marehemu kama atazikwa Kijiji cha Myangayanga alikozikwa baba yake.
Mwananchi iliyokuwa nyumbani kwa marehemu na kushuhudia vilio na simanzi na wengi wamekuwa wakizidisha vilio hasa kutokana na mke wake kuwa na kichanga kwani alikwenda kujifungua nyumbani kwao Zanzibar.
Kwenye Kambi ya Majimaji, Nachingwea ilifahamika kuwa Koplo Chukilizo ambaye alikwenda Darfur kama fundi wa magari ya deraya, ni mwenyeji wa Kigoma na kwamba huenda akasafirishwa kwenda huko.
Baba mkwe ambaye marehemu alizaa na mwanawe alisema: “Taarifa nimezipata jioni hii, tulikuwa na wasiwasi lakini tukathibitisha

No comments: