DAKTARI anayedaiwa kuwa bandia amekamatwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, akiwa na vitambulisho bandia vya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) akisomea Shahada ya Pili.
‘Daktari’ huyo ambaye amekuwa akitafutwa na uongozi wa
chuo kwa zaidi ya mwaka alikamatwa jana asubuhi akiwa hospitalini hapo karibu na
jengo kilimo kitengo cha meno.
Katika kitambulisho chake cha kupigia kura
anatambulishwa kwa jina la Dismas John Macha aliyezaliwa mwaka 1979 Kilimanjaro
na anaishi maeneo ya Upanga Magharibi, Dar es Salaam.
Gazeti hili, lilimshuhudia mtuhumiwa huyo akiwa katika
kituo cha usalama cha Muhas na kupekuliwa na askari Polisi wa Muhimbili, Anthony
Mwamatepela na kukutwa akiwa na vifaa vya udaktari .
Baadhi ya vifaa alivyokutwa navyo ni pamoja na koti
jeupe la udaktari na stetoskopu ambacho ni kifaa cha kusikilizia mapafu
yanavyofanya kazi na mapigo ya moyo.
Pia alikuwa na begi jeusi lenye aina mbalimbali za
dawa, vitambulisho na karatasi nyingi, lakini alipoulizwa alidai kuwa hizo ni
dawa zake.
Macha alikutwa pia na vitambulisho vitatu tofauti,
kimoja kikimtambulisha kuwa mwanafunzi wa Muhas wa Shahada ya Pili ya Udaktari
(Masters of Medicine ) yenye jina la Macha Dismas kikionesha kusajiliwa kwa
namba 60520/2011 na kumaliza muda wake Septemba 30 mwakani. Kitambulisho kingine
kilimtambulisha kwa jina la Macha Rogers anayesoma Shahada hiyo hiyo ikionesha
kuwa anamaliza masomo yake mwakani.
Alikutwa pia na kitambulisho kinachomwonesha kuwa
mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza na kadi ya anuani yenye jina la Amos Nnko ambaye
ni Ofisa Rasilimaliwatu wa Chuo hicho.
Akizungumzia alivyomkamata askari wa chuo hicho,
Fulgence Semfukwe alisema walimkamata baada ya kupata taarifa za yeye kuwa
maeneo hayo na kupanga mbinu za kumkamata.
Alisema saa 4.45 asubuhi jana alimkuta kwenye jengo la
meno na kumwomba kwa nafasi yake ya udaktari amsaidie tatizo lake na hivyo
waongee pembeni, naye bila wasiwasi akakubali. Alimwuliza anatibu magonjwa gani
naye kumjibu anatibu maradhi ya aina nyingi na kumwomba kitambulisho na yeye
kumpa cha kwake.
Baada ya hapo alishituka na kudai kuwa ni daktari wa
Mwananyamala na amekuja hapo kwa ajili ya kuona wagonjwa wake wa dharura ndipo
alipokamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi.
Alisema amekuwa akiwachenga kwa muda mrefu kutokana na
kuwa kila walipopewa taarifa yuko wodi au sehemu Fulani hawakumkuta kwani
walipishana naye baada ya kuvua koti na kuweka kwenye begi lake
jeusi.
Akizungumza na gazeti hili, Macha limweleza mwandishi
wa habari hizi kuwa yeye ni mwanafunzi ambaye anaelewa masuala yote ya matibabu,
lakini alifeli chuoni hapo mwaka jana.
Alidai kuwa dawa alizokutwa nazo ni zake kwani ana
matatizo katika njia ya mkojo na kifua huku akiamua kufanya hivyo kutokana na
ugumu wa maisha.
“Uwezo wa kutibu ninao na nimesoma katika chuo hiki,
lakini mwaka jana nilifeli ndiyo maana nikaamua kuwa hivi,”
alisema.
Ofisa Uhusiano wa Muhas, Hellen Mtui alisema kutokana
na kukamatwa na nyaraka akijitambulisha kuwa mwanafunzi wa ‘Masters of
Medicine’, ambaye anaweza kutibu watu hawana uhakika na idadi ya watu ambao
ameshatapeli hospitalini hapo.
Kuhusu kusoma Muhimbili, Mtui alikana akisema baada ya
kupekua nyaraka za chuo hawakubaini jina la mwanafunzi wa aina hiyo na katika
vyeti vyake bandia vinaonesha kusainiwa na Mkuu wa Chuo aliyekuwapo kabla chuo
hakijapanda hadhi na kuwa chuo kikuu.
Mtui alisema baada ya kumkamata na kumpiga picha akiwa
na mavazi ya udaktari, kumpekua na kumhoji walimpeleka katika kituo cha Polisi
cha Selander Bridge kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment