Friday, May 17, 2013

Wanawake Iran hawawezi kugombea Urais

Wanawake nchini Iran wanaweza kugombea nyadhifa za bunge
Baraza la kikatiba nchini Iran limeamua kuwa wanawake hawawezi kugombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 14 mwezi Juni.
Mohammad Yazdi, Afisaa mmoja wa baraza la Guardian, alisema kuwa katiba hairuhusu wanawake kushiriki katika uchaguzi huo.
Wanawake thelathini woliokuwa wamejisajili kugombea urais, walikuwa na matarajio madogo sana kuwa wangeruhusiwa kushiriki.
Aidha baraza la Guardian, linakabiliwa na jukumu la kuwakagua wagombea kulingana na misingi ya kidini.
Wachunguzi wanasema kuwa katiba haijafafanua vyema kuhusu wanawake kushiriki katika uchaguzi wa urais nchini humo.
Hata hivyo, ufafanuzi uliotolewa hivi karibuni kuhusu swala hilo ndio unafikisha kikomo mjadala huo.
Shirika la habari la Mehr, lilimnukuu bwana Yazdi akisema kuwa sheria hairuhusu mwanamke kugombea urais na kuwa jina la mwanamke halipaswi kuwa katika katarasi ya kupigia kura.
Wanawake hata hivyo wanaweza kugombea nyadhifa za bunge na wamekuwa wakihudumu kama wabunge.
Rais wa sasa Mahmoud Ahmadinejad, hawezi kugombea muhula wa tatu kulingana na sheria za kikatiba na watu 686, wamejisajili kugombea nafasi hiyo.
Orodha ya mwisho ya wagombea itatangazwa Jumanne huku watu wachache wakiteuliwa kugombea.
Katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2009,wagombea 475 walijisajili kushiriki uchaguzi huo lakini baraza la kikatiba la Guardian, iliweza tu kuwaidhinisha watu wanne kugombea.
Matokeo ya uchaguzi yalizua maandamano baada ya upinzani kusema yalihujumiwa.
Wangombea wanaounga mkono mageuzi, Mir Hossein Mousavi na Mehdi Karroubi, walipewa kifungo cha nyumabni kila mmoja.

No comments: