Mtoto wa kiume wa kiongozi wa
Libya aliyeondolewa madarakani, marehemu Kanali Muammar Gaddafi, Saif al
- Islam, amefikishwa mahakamani kwa dakika chache katika mji wa Zintan
kujibu mashtaka ya uhalifu.
Kesi inayomkabili inahusiana na ziara ya mwaka
jana ya wakili kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambaye
anatuhumiwa kumpatia taarifa Bwana al - Islam.Al - Islam pia anashtkiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita yaliyotekelezwa wakati wa vuguvugu la mageuzi mwaka 2011. Libya na ICC zote kwa pamoja zinadai kuwa na haki ya kusikiliza kesi hiyo.
Alipofikishwa mahakamani siku ya Alhamisi, Bw. Al - Islam kwa mara ya kwanza alipewa wakili wa kumtetea.
Mhariri wa Habari za Nje wa BBC, John Simpson aliyeko mjini Zintan anasema, Bw. Al - Islam alipoulizwa kama ni mwenye afya njema alijibu ndio, huku akionesha ishara ya dole gumba.
Mashtaka yanayomkabili
Anakabiliwa na mashtaka ya kushiriki katika kubadilishana taarifa, kupata nyaraka ambazo zinatishia usalama wa taifa na kuidharau bendera ya taifa.Ushahidi uliwasilishwa kwa dakika chache wakati kesi inasikilizwa ikiwemo kalamu yenye kamera na saa ya mkononi, ambayo mwendesha mashtaka anadai ilitumika kupenyeza taarifa hizo haramu.
Mnamo Juni mwaka jana, wakili wa ICC, Melinda Taylor na watumishi wengine watatu wa ICC walikamatwa na kushikiliwa kwa wiki tatu baada ya kumtembelea Bw. Al - Islam.
Bi. Taylor anatuhumiwa kumpatia kwa siri Bw. Al - Islam barua yenye herufi za siri kutoka kwa msaidizi wa zamani aliye uhamishoni, Mohammed Ismail.
Watumishi hao wanne hatimaye waliachiliwa huru na kukabidhiwa The Hague na hawatarajii kurejea Libya kukabili mashtaka.
Al - islam amekuwa akishikiliwa mjini Zintan tangu kikosi kutoka mji huo kimkamate Novemba 2011.
Wakili wake raia wa Uingereza, John Jones, ameelezea kukamatwa kwa Al - Islam kama Guantanamo ya Libya, na kuongeza kuwa hana mpango wa kumtembelea Al - Islam mjini Zintan.
No comments:
Post a Comment