Wednesday, May 22, 2013

Nigeria kuwaachiliwa wanawake washukiwa

Wapiganaji wa Boko Rama wamewateka nyara wanawake na wasichana
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, ameamuru kuachiliwa kwa wanawake wote waliokamatwa kwa kuhusishwa na vitendo vya kigaiidi. Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka wizara ya ulinzi.
Kulingana na wizara hiyo, uamuzi huo ulilenga kuimarisha juhudi za amani nchini Nigeria.
Jeshi linaendesha operesheni katika majimbo matatu ambako sheria ya hali ya hatari ilitangazwa wiki jana ili kuwezesha jeshi kupambana vilivyo na wapiganaji wa kiisilamu wa Boko Haram.
Kundi hilo lilisema kuwa halitawaachilia wanawake na watoto waliowateka nyara ikiwa serikali haitafanya mazungumzo nao
Zaidi ya watu 2,000 wamefariki nchini Nigeria katika mashambulizi yaliyofanywa na Boko Haram tangu mwaka 2009 wakitaka kuundwa kwa jimbo litakalofuata sheria za kiisilamu.
Mapema mwezi huu kundi hilo lilitangaza kuwateka nyara wanawake na wasichana wadogo kulipiza kisasi hatua ya jeshi kuwakamata wake za wanamgambo hao.
Wapiganaji hao walisema kuwa wanafanya wanawake hao kuwa watumishi wao.
Wizara ya ulinzi ilisema kuwa wanawake kadhaa waliokamatwa kama washukiwa wa ugaidi , watakabidhiwa kwa polisi ili kupewa mafunzo ya kurekebisha tabia yao kabla ya kuachiliwa.
Duru zinasema kuwa uamuzi wa rais Jonathan, haujaonda fursa ya kufanyika mazungumzo kati ya serikali na wapiganaji wa Boko Haram, licha ya kuazisha operesheini ya kijeshi dhidi ya wapiganaji hao.
Rais Goodluck, alitangaza sheria ya kutotoka nje katika majimbo matatu ya Kaskazini Mashariki, Borno, Yobe na Adamawa, ambako Boko Haram lina ngome zake kuu.
Wanajeshi 2,000, walipelekwa katika maeneo hayo wiki jana, ikiwa ni moja ya operesheni kubwa zaidi ya kijeshi dhidi ya Boko Haram kuwahi kushuhudiwa.
Jeshi limesema kuwa pia limesema lilitumia ndege za kivita kushambulia ngome za kundi hilo.
Waziri wa mambo ya nje nchini Marekani John Kerry, ameitaka serikali ya Nigeria kuhakikisha kuwa jeshi halikiuki haki za binadamau wakati likiendesha kampeini hiyo dhidi ya Boko Haram.
Bwana Kerry alisema kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha jeshi limekiuka haki za binadamu.

No comments: