Kesi ya mauaji dhidi ya
mwanajeshi wa Uganda imeendelea nje ya kambi yake ya Bombo umbali wa
kilomita 40 kaskazini mwa mji mkuu wa Kampala.
Mwanajeshi huyu anadaiwa kuwapiga risasi na kuwauwa watu 10 mwezi mmoja uliopita nje ya kambi ya kijeshi ya Bombo.Hata hivyo baadhi wanadai kuwa wanajeshi haswa wanaotoka katika maeneo ya hatari hawapewi huduma za kuwatuliza kisaikolojia jambo ambalo limekanushwa na jeshi.Mwandishi wetu wa Kampala Siraj kalyango na maelezo zaidi.
Mwanajeshi huyo, Private Patrick Okot,anakabiliwa na mashtaka kadha yakiwemo, mauaji, wizi wa kutumia nguvu pamoja na kushindwa kutumia vizuri mali ya jeshi.
Katika kikao cha leo, mahakama ya kijeshi imearifiwa kuwa mshatakiwa hana kasoro yoyote ya kiakili.
Shahidi namba 16 ambaye ni daktari wa upasuaji katika hospitali kuu ya Mulago aliyefanyia uchunguzi miili yote ya waathirika ,ameiambia mahakama kuwa miili yote 10 ilikuwa na majeraha ya risasi.
Baadhi ya makundi yasiyo ya kiserikali yanadai kuwa matukio mbalimbali ya wanajeshi hasa kupiga risasi raia,baada ya kurejea kutoka vitani, kunaashiria matatizo yaliyopo ndani ya jeshi ukiwemo ukosefu wa kuwapa huduma za kisaikolojia .
Maelezo zaidi kuihusu kesi hiyo inayomkabili mwanajeshi huyo ni kuwa ilianza kusikilizwa wiki mbili zilizopita na imepangwa hukumu itolewe katika muda wa siku 21.
Hii italazimu mahakama ya kijeshi kufanya vikao vyake kwa siku tatu mfululizo kila wiki kuanzia Jumatatu, Jumanne na Jumatano.
No comments:
Post a Comment