Tuesday, December 18, 2012

Tumuunge mkono Mrisho Ngassa kukomesha 'mahakama ya ndizi'

Maoni ya Katuni
Winga Mrisho Ngassa wa timu za taifa za Kilimanjaro Stars ya Bara na Taifa Stars alilazimika kujificha wiki hii, mwenyewe amedai alikuwa mapumzikoni jijini Arusha, ili kumkwepa mwakilishi wa klabu ya El Mereikh ya Sudan aliyekuwa Dar es Salaam kukamilisha safari yake ya kwenda nchini humo kufanyiwa uchunguzi wa afya ili aweze kusajiliwa huko.

Ngassa ambaye kimsingi ni mchezaji wa klabu ya Azam anayekipiga kwa mkopo katika timu ya Simba kwa sasa anaendelea na mazoezi ya Taifa Stars inayojiandaa kuikabili Zambia Jumamosi ijayo, lakini chini ya wingu la lawama kutoka pamoja na mashabiki wa soka nchini wanaoamini amechemsha kuikacha El Mireikh, baadhi ya viongizi wa Simba na Azam.

Wamemponda, viongozi hao, wakidai kuwa kitendo hicho cha Ngassa kimelitia aibu taifa na huenda kikafunga milango ya wachezaji wengine nchini kutakiwa na timu za nje, hasa Sudan.

Bila kuangalia maslahi ambayo angelipwa Ngasa kwa kwenda kuchezea timu ya El Mireikh, Nipashe tunafahamu, mchezaji huyo angekuwa amepata nafasi nzuri 'mara 800' ya kujiendeleza kisoka na kimaslahi kutokana na anga ambayo timu hiyo ya Sudan ipo.

Kwa kulinganisha rekodi za timu za Simba na Azam kwenye michuano ya klabu ya Afrika, na unapoongeza ubabaishaji unaoonekana kuwepo katika utawala wa timu mbili hizo, ni wazi Ngassa alikuwa anakwenda kulelewa katika mazingira bora zaidi kama mchezaji na, kama ambavyo tumesema tayari, Taifa Stars na yeye mwenyewe angenufaika mno.

Mfumo wa ufundishaji katika klabu ya El Mereikh, kwa vyovyote, Nipashe tunaamini, upo juu na ndiyo maana kwa kuongeza na ubora wa wachezaji walio huko tayari kuliko wale wa Simba na Azam, timu hiyo ilifika nusufainali ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika ambalo Simba ilitupwa nje na El Shandy kabla. 

Aidha, kutokana na kufanya vizuri mara kwa mara kwa El Mireikh kwenye michuano ya klabu ya Afrika kulinganisha na Simba, palikuwa na dirisha kubwa zaidi la kujiuza 'majuu' na kupata pato kubwa zaidi kiuchumi kwa Ngassa katika timu hiyo ya Sudan kuliko hapa nyumbani.

Lakini, wanaomlaumu, wamesikia kilio chake kikuu KILE KILE kwa mara ya pili?

Wakati Ngassa akiuzwa kwa mkopo kwenda Simba, katika usajili wa msimu huu mwishoni mwa mwaka jana, alilalamika kuwa biashara hiyo ilifanywa bila ridhaa yake na kwamba anajiona kama "mafungu ya nyanya".

Pamekuwa na madai kutoka kwa viongozi wa klabu zake mbili hizo, sasa, kuwa Ngassa alizungumza na El Mireikh, na kufikia makubaliano ya awali nayo, akiwa nchini Uganda katika Kombe la Chalenji la Afrika Mashariki na Kati.

Lakini tunaamini Nipashe, hayo yalikuwa ni mazungumzo na makubaliano yaliyofikiwa kutokana na shinikizo.
Yalikuwa ni maafikiano yaliyotokana na shinikizo kwa kuwa mchezaji huyo aliwekwa katika kona ambayo mbaya, kwa kuwa hakuwa ametaarifiwa hapo kabla.

Katika soka la kulipwa, kama ambalo Ngassa yumo, mchezaji ni mali ya klabu na Nipashe tunafamu hilo vizuri. Sana.

Lakini tunafahamu vizuri sana pia, Nipashe, kuwa mchezaji si fungu la nyanya. Kwamba ridhaa yake, kama ilivyo ridhaa ya klabu, inahitajika katika masuala ya uhamisho.

Hivyo badala ya Azam kuruhusu El Mireikh kufanya mazungumzo na Ngassa nchini Uganda, lilikuwa ni jukumu la uongozi wa klabu hiyo ya ligi kuu ya Bara kumuuliza kwanza mchezaji huyo kama atapenda kuzungumza nayo.

Kutofikia makubaliano na mchezaji husika kabla ya kumruhusu Ngassa kufanya mazungumzo na El Mireikh, tunaona Nipashe, ni kujaribu kumuuza mchezaji huyo bila ridhaa yake kwa mara ya pili, wakati mchezaji hapaswi kuuzwa kama mkungu wa ndizi katika 'mahakama ya ndizi', Mabibo.  



 
CHANZO: NIPASHE

No comments: