Friday, December 7, 2012

Hoteli inatiririsha kinyesi baharini

Hoteli ya Double Tree iliyopo Masaki, jijini Dar es Salaam imebainika kutiririsha kinyesi na majitaka kwenda baharini baada ya Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Charles Kitwanga, na maofisa waandamizi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc), kufanya ziara kushtukiza hotelini hapo jana.
Hoteli  ya Kitalii iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, yenye hadhi ya nyota tano imeumbuka baada ya kubainika kumwaga maji ya chooni baharini.

Madudu ya hoteli hiyo inayotambuka kama Double Tree by Hilton, yamebainika baada ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Charles Kitwanga, pamoja na maofisa waandamizi kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (Nemc).

Ziara hiyo imebaini kwamba mfumo wa majitaka ya hoteli hiyo haujajengwa vizuri kuruhusu maji hayo kusafishwa kabla hayajamwagwa au kuingizwa kwenye mfumo wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco).

Kitwanga na maofisa hao wa Nemc walifika kwenye hoteli hiyo majira ya saa 7:00 mchana na kuhoji mfumo wa majitaka pamoja na sababu za hoteli hiyo kujengwa hadi baharini.

Mameneja wa hoteli hiyo walimweleza Naibu Waziri kwamba maji hayo yanahifadhiwa vyema na kisha kuzolewa kwa magari ambayo huenda kuyamwaga kwenye mabwawa ya majitaka.
 Hata hivyo, Kitwanga alihoji linapopita gari la kuja kuchukua maji hayo kwa kuwa eneo zima limezungukwa na majengo pamoja na ukuta usioruhusu gari kupita.

Baada ya kuendelea kukagua, ndipo ilibainika kwamba uchafu wote wa hoteli hiyo na hasa maji ya chooni yanamwagwa baharini.

"Tulichoona hapa ni kinyesi kabisa, harufu ya maji ya chooni inatoka halafu hawa wanatudanganya eti ni mtiririko wa maji wa kawaida, hali hii haikubaliki," alisema Kitwanga.

Kitwanga alisema serikali inawahamasisha wawekezaji waje kuwekeza nchini, lakini kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, vinginevyo itawachukulia hatua stahiki.

Alimweleza Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Sven Lippinghof, kwamba kumwaga kinyesi baharini ni suala lisilovumilika na kumtaka kuzingatia sheria ya mazingira na nyinginezo ili kulinda afya ya viumbe wa baharini na za wananchi.

Naibu Waziri huyo aliitaka Nemc kufuatilia kwa kina usitishwaji wa kumwaga maji hayo na kumpa mwekezaji huyo wiki moja kwamba hadi Ijumaa ijayo awe amefanya marekebisho ya kina.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Nemc, Manchere Heche, aliitaka hoteli hiyo kusitisha kumwaga maji hayo baharini kuanzia jana na kumwandikia barua ya kusisitiza amri hiyo.
 Alisema kuanzia leo, Nemc itafanya ukaguzi katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba agizo hilo linatimizwa.

"Napenda tu nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba suala la afya ya wananchi ni la msingi na muhimu, leo hii (jana) kwamba Nemc inawataka msitishe kumwaga haya maji na nitawaandikia barua leo kusisitiza hili," alisema Heche.

Alisema: "Afya za watu haziwezi kusubiri muda, na tutawatoza faini kwa uchafuzi huu wa mazingira."

Kwa upande wake, Lippinghof alisema atatekeleza maagizo hayo ya Nemc na kwamba suala la kuzingatia sheria halina mjadala.

Alisema atawasilisha pia maagizo hayo kwenye kikao cha bodi ya wakurugenzi wa hoteli hiyo kwa hatua kubwa zaidi.

Awali, ziara hiyo ilifanyika pia kwenye hoteli ya Giraffe ambayo ilibainika kuchafua bahari na kuagizwa kufanya usafi kila siku.

Kadhalika, Waziri Kitwanga aliiagiza Nemc kusimamisha ujenzi wa hoteli ya Blue Pearl inayojengwa karibu na Giraffe kwa kuwa imejenga ukuta baharini na hivyo kuinyima bahari kupumua.

Katika ziara hiyo, kiwanda cha Coca cola Kwanza ndicho pekee kilichoonekana kuzingatia sheria ya mazingira kwa kujenga mfumo wa kusafisha maji yenye sumu kabla hakijayamwaga.

Maeneo mengine ambayo yalitembelewa na Naibu Waziri huyo ni kiwanda cha dawa Sheyls Pharmacetical, hoteli za Whitesands na Corol Beach ambazo zilipewa maelekezo madogo baada ya kubainika kutotimiza masharti ya sheria ya mazingira.
CHANZO: NIPASHE

No comments: