Tuesday, December 18, 2012

Barabara, vituo vya daladala Dar kubadilishwa mwakani

Katika  kuhakikisha msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar es Salaam unapungua, serikali kupitia halmashauri za jiji hilo, imepanga kufanya mabadiliko ya mzunguko wa magari kuanzia mwakani.

Taarifa kuhusiana na mabadiliko hayo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam kupitia wasimamizi wa mradi huo ambao ni Ofisi ya Katibu wa Mkoa, Halmashauri ya Jiji na Halmashauri ya Ilala, kwenye mkutano wa kufanya tathmini ya mradi wa kuboresha usafiri katika jiji hilo.

Baadhi ya malengo ya kufanya mabadiliko hayo yameelezwa kuwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji, kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya mradi wa magari yaendayo haraka ‘BRT’ (Dart) na kuwezesha sehemu ya Barabara ya Morogoro itumike kwa mabasi ya mradi huo pekee.

Kuanza kwa mabadiliko hayo kutafanya daladala zote zinazotoka maeneo ya  Mbagala Rangi Tatu, Temeke, Gongo la Mboto, Vingunguti, Tabata/Segerea kwenda Posta, kumalizia safari zake katika kituo cha Stesheni.

Mabadiliko hayo pia yamegusa daladala zote zinazokwenda Posta kupitia barabara za Ali Hassan Mwinyi na Morogoro, ambazo kwa sasa zitakuwa zinahitimisha safari zake katika kituo kipya cha YMCA.

Kwa upande wa mabadiliko ya barabara, daladala zote zilizokuwa zinapita katika barabara za Sokoine na Uhuru, zitatakiwa kurudi kupitia barabara ya Maktaba/Azikiwe huku barabara itakayokuwa ya njia moja ni ile ya Aggrey inayoelekea Barabara ya Bibi Titi.

Aidha, barabara ambazo zitatakiwa kugeuza mwelekeo ni pamoja na zile za mitaa ya Samora na Sokoine pekee.

Akizungumza na NIPASHE jana, baada ya kipindi cha kwanza cha mkutano huo kumalizika, Katibu wa mradi unaosimamia makubaliano ya uboreshaji usafiri na sera katika Jiji la Dar es Salaam, Emma Manyanga, alisema sehemu ya pili ya mkutano huo ililenga kujadilili mabadiliko hayo yanayotarajiwa kuanza mwakani na kuongeza kwamba siku rasmi ya uzinduzi itawekwa hadharani kupitia vyombo vya habari.

Naye Mhandisi Wizara ya Ujenzi, Ven Ndyamukama, aliyataja baadhi ya mafanikio tangu kuanza kwa mradi huo wa kuboresha usafiri jijini Dar es Salaam miaka miwili iliyopita kuwa ni pamoja na kutambua matatizo yakiwamo ufinyu wa barabara na mizunguko yake.

Alisema utekelezaji unaoonekana bado kutokana na uhaba wa rasilimali kama vile fedha.

Kwa mujibu wa Ndayamukama, mkutano huo uliojumuisha kamati ya mradi huo, timu ya wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (Jica), ulilenga kufanya tathmini ya mradi huo ambao ni wa awamu ya kwanza ulioanza miaka miwili iliyopita na kutarajiwa kumalizika Desemba, mwaka huu.

Kwa upande wake, Mhandisi Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam, Swalehe Nyenye, alisema awamu ya pili ya mradi inatarajiwa kuanza rasmi mwakani baada ya Serikali ya Japan kwa ajili ya udhamini.

Nyenye alisema dola milioni 300 za Marekani zinatakiwa kukamilisha mradi huo  huku dola 90 zikiwa zinasubiriwa kuchukuliwa kutoka Benki ya Dunia (WB).

Mjadala mwingine uliotawala kwenye mkutano huo ni pamoja na kutengenezwa kwa sera ya usimamizi wa usafiri maeneo ya mijini.

Akifungua mkutano huo, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Jumanne Sagini, alisema tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, ni moja ya changamoto kubwa nchini.

Sagini alisema hiyo ni kwa sababu ya inapoteza mapato ya kiuchumi kutokana magari kutumia muda mrefu barabarani na wakati mwingine mizigo kuchelewa kuondolewa kwa wakati bandarini.


 
SOURCE: NIPASHE

No comments: