Saturday, December 1, 2012

Polisi wamwaga tena damu ya raia

  *Yu mahututi wodini Muhimbili
  *Vurugu zatanda, barabara yafungwa
Askari Polisi wakilinda doria eneo la Tegeta kwa Ndevu baada ya kutokea vurugu ambapo mtu mmoja alidaiwa kujeruhiwa na pilisi Jijini Dar es Salaam jana na kukimbizwa hospitali kwa matibabu.
Vurugu kubwa zilizohusisha ufyatuaji wa mabomu ya machozi na risasi za moto kati ya askari wa Jeshi la Polisi na wananchi, jana zilizuka katika eneo la Tegeta, jijini Dar es Salaam na kusababisha kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 17 kujeruhiwa kwa risasi kichwani.

Kijana huyo amefahamika kwa jina la John Massawe, ambaye alikumbwa na mkasa huo alipokuwa dukani akiuza magodoro.

Vurugu hizo zilizuka majira ya saa 4:45 asubuhi katika eneo maarufu kama “Tegeta kwa Ndevu”.

Habari kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa vurugu hizo zilizodumu kwa takriban dakika 15, zilisababishwa na baadhi ya maofisa wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Maofisa hao wa Tanroads wanadaiwa kufika katika eneo hilo wakiwa na magari ya kunyanyua na kuvuta vitu vizito, maarufu kama “Break Down” na kutaka kuyakamata magari yaliyokuwa yameegeshwa pembezoni mwa barabara.

Kwa mujibu wa habari hizo, baada ya kufika katika eneo hilo, maofisa hao wa Tanroads walianza kuyakamata magari hayo.

Kitendo hicho kilipingwa na wananchi, ambao walianza kuwazuia maofisa hao wa Tanroads, huku wakiwazonga.

Hali hiyo ilisababisha askari polisi kuitwa, ambao baada ya kufika, waliwaamuru wananchi kutawanyika, lakini amri hiyo ikapuuzwa.

Kutokana na amri hiyo kupuuzwa, askari hao walianza kufyatua risasi hewani pamoja na mabomu ya machozi na kuzua tafrani na hofu kubwa katika eneo hilo.

Katika tafrani hiyo, mmoja wa askari polisi anadaiwa kumpiga mtoto huyo risasi kichwani na kudondoka hapo hapo.

Milio ya risasi za moto iliendelea kurindima katika eneo hilo, huku mtoto huyo akiwa amelala chini akitokwa damu nyingi bila ya msaada wowote.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao walianza kukimbia hovyo, huku wafanyabiashara wa maduka yaliyopo karibu na tukio zilipotokea vurugu hizo wakilazimika kuyafunga.

Baada ya dakika 15 kupita, hali ilirejea kuwa ya kawaida na wananchi walianza kujikusanya makundi makundi wakijadili mkasa huo.

Majira ya saa 7:52 mchana wananchi hao waliamua kufunga barabara kwa kutumia magogo, madaraja ya mbao na matenga.

Hatua hiyo ilisababisha magari kushindwa kuendelea na safari zake na hivyo kusababisha msongamano mkubwa wa magari kwa muda katika eneo hilo.

Dakika chache baadaye, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Wazo, Mponjoli Mponjoli, akiwa ndani ya gari la polisi lenye namba PT 2083, alifika katika eneo hilo.

Baada ya kufika, alishuka kwenye gari lake na kuanza kuwasihi wananchi hao kuacha vurugu na kuwataka wawe na subira.

Pia lilifika gari lingine la polisi aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili MX 54 UKH, likiwa na askari, ambao walishuka na kuanza kuondoa vizuizi.

Hata hivyo, licha ya Mponjoli kuwasihi hivyo, wananchi hao walipuuza na kuanza kuimba nyimbo za kutaka haki itendeke.

Sanjari na kuimba nyimbo hizo, wananchi hao waligoma kuondoka kwa madai ya kutaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika waliosababisha vurugu hizo.

Hali hiyo ilionekana kumzidi Mponjoli na hivyo, iliilazimu makao makuu ya jeshi hilo kuongeza nguvu kwa kumtuma  Mkuu wa Operesheni maalum wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro, ambaye alifika eneo hilo na kuwasihi wananchi hao kuwa watulivu na kuwaahidi kuwa upelelezi wa tukio hilo utafanyika.

Hata hivyo, wananchi walioonekana kuwa na jazba, walisema wanaostahili kulaumiwa ni Tanroads kwa kushindwa kuweka vibao katika sehemu zisizoruhusiwa kuegesha magari.

“Hii inaonekana kama biashara. Yaani hawa watu wanapokuta gari lako bila kuuliza wanaita ‘break down’ na kulifunga. Ukilipa pesa wanayotaka wanakuachia. Kwanini hawaweki vibao vya kuonyesha kuwa sehemu fulani haziruhusiwi kupaki magari?” alihoji mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Boniface Masumbuko.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema tukio hilo lilitokea baada ya Kampuni ya Udalali ya Mwakinga kukamata gari lililokuwa limeegeshwa sehemu hiyo ambayo hairuhusiwi kuegesha magari.

Kamanda Kenyela alisema baada ya kukamata gari hilo, wananchi walianza kuwarushia mawe na kusababisha askari polisi kufika kwa ajili ya kutoa msaada.

Alisema hata baada ya polisi kufika, wananchi waliendelea na vurugu za kurusha mawe na katika vurugu hizo kuna mtu alijeruhiwa.

Hata hivyo, alisema taarifa za kuwa kuna mtu aliyekufa katika vurugu hizo si za kweli, bali alijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mwananyamala, ambako anaendelea na matibabu.

HOSPITALI YA MWANANYAMALA WAZUNGUMZA

Katibu wa Afya wa Hospitali ya Mwananyamala, Edwin Bisakala, alithibitisha kuwapo kwa majeruhi huyo hospitalini hapo.

Alisema walimpokea kijana huyo majira ya saa 6:00 mchana na kumpatia huduma ya kwanza.

Bisakala alisema, mtu huyo alipata majeraha makubwa kichwani na walimpatia huduma ya kwanza na kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)  kwa matibabu zaidi.

“Ni kweli tumempokea majeruhi wa aina hiyo. Tulimtibu na kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu. Kwa kuwa alikuwa anahitaji matibabu zaidi,” alisema Bisakala.

HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI WAZUNGUMZA

Afisa Habari wa MNH, Aminieli Eligaesha, aliliambia NIPASHE jana jioni kuwa walimpokea mgonjwa huyo kutoka Hospitali ya Mwanayamala majira ya mchana akiwa katika hali mbaya na kupelekwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) hospitalini hapo.

Alisema hadi jana hali yake ilikuwa mbaya na madaktari walikuwa wanaendelea kumpatia matibabu zaidi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: