*********
Habari
za uhakika kutoka ndani ya Jeshi hilo zimedokeza kuwa Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema anatarajiwa kustaafu mwezi
ujao na haijafahamika kama ataongezewa mkataba ama la.
Vyanzo
mbalimbali vimedai kuwa japokuwa IGP Mwema anasita kukubali kuongezewa
muda, lakini Rais Jakaya Kikwete anaonelea aongezewe muda ili wamalize
pamoja uongozi wao mwaka 2015.
IGP
Mwema ambaye alikuwa Ofisi ya Polisi wa Kimataifa (Interpol) Jijini
Nairobi, Kenya, aliteuliwa kushika wadhifa wake huo mwaka 2006 na Rais
Kikwete, kumrithi Omar Mahita ambaye alistaafu.
Habari
zinasema endapo IGP Mwema hatapewa mkataba wa ama miaka miwili, basi ni
dhahiri Rais Kikwete atakuwa na kibarua kigumu cha kuanza mchakato wa
kumtafuta mrithi wake.
IGP
Mwema anachukuliwa kama mmoja wa viongozi wa juu wa Jeshi hilo
aliyelifanyia mapinduzi makubwa aliposhika madaraka hayo, ikiwamo kuja
na dhana ya ulinzi shirikishi ama Polisi Jamii.
Tayari
mabadiliko hayo yameaanza kufanyika kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kinondoni jijini Dar es Salaam, Charles Kenyela kuhamishiwa makao makuu
ya jeshi hilo.
Taarifa
zaidi zimepasha kuwa nafasi nyingine ya juu ambayo kuna dalili ya
kuwepo kwa mabadiliko ni ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(DCI), inayoshikiliwa na Robert Manumba.
Wanafunzi Bora wazungumzia matokeo
*****
Mwanafunzi
bora wa kwanza kitaifa katika matokeo yaliyorekebishwa ya mtihani wa
kidato cha nne uliofanyika mwaka 2012, Said Irando kutoka Shule ya
Sekondari Feza ya jijini Dar es Salaam, ameeleza kushangazwa na matokeo
hayo kwa kuwa hakuyatarajia.
Mwanafunzi
huyo ambaye tayari ameshaanza masomo ya Kidato cha Tano katika Shule ya
Sekondari Feza, alisema kuwa ingawa alisoma kwa bidii lakini hakudhani
kama angeweza kushika nafasi ya kwanza kitaifa na kwamba anamini
mafanikio yake kitaaluma yana ‘mkono wa Mungu’.
“Sikutegemea
kabisa kuwa mwanafunzi bora, ingawa nilisoma kwa bidii kubwa nia yangu
ilikuwa ni kutaka kufaulu tu; Ni Mungu amenisaidia,” alisema Irando.
Alisema
kujituma katika masomo, mazingira mazuri ya kusomea na upatikanaji wa
vifaa muhimu vya kujifunzia ndiyo yaliyomwezesha kusoma na kufanya
vizuri.
Irando
ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto watatu, alisema
kurekebishwa kwa matokeo ya kidato cha nne kulibadilisha alama za
matokeo yake kutoka Daraja la kwanza akiwa na alama tisa hadi saba,
zilizomfanya kuwa mwanafunzi bora kitaifa na mwafunzi bora wa kwanza
kati ya wavulana kumi bora pia kitaifa.
Mwanafunzi
huyo alibainisha kuwa pamoja na wazazi wake kuwa ni wafanyabiashara,
yeye anatamani kuwa mhandisi ingawa bado hajajua atakuwa mhandisi katika
tasnia gani.
“Natamani sana kuwa mhandisi hiyo ndiyo ndoto yangu ingawa bado sijajua nitakuwa mhandisi wa sekta gani,” alisema Irando.
No comments:
Post a Comment