Friday, June 7, 2013

USHIRIKI DARFUR MIKONONI MWA SERIKALI- TENGA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.
Tenga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF, alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa tamko.
“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.
“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.
“Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”
Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.
Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.
“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,” alisema Tenga.
“Lakini napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu Mkuu wa CECAFA (Nicholas Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.
Alisema watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.
“Mhe. Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.
“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”
Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.
“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,” alisema.

“Sasa ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA.”
TAIFA STARS SASA INAJITOSHELEZA- TENGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kuiwezesha timu ya taifa, Taifa Stars kuondokana na matatizo na kuwaomba Watanzania kuiombea timu ili ifanye vizuri katika mechi yake ya kesho (Juni 8 mwaka huu) dhidi ya Morocco mjini Marrakech.
Stars, ambayo inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake la mashindano ya awali ya Kombe la Dunia ikiwa nyuma ya Ivory Coast kwa tofauti ya pointi moja, inacheza na Morocco katika mechi ya nne itakayofanyika Marrakech baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Dar es Salaam mwezi Machi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa tangu kuanza kwa udhamini, TFF haijawahi kupata udhamini mkubwa kama wa Kilimanjaro Premium Lager ambayo imeingia mkataba wa miaka mitano wa kuidhamini Stars wenye thamani ya dola milioni 10 za Marekani.
“Katika kipindi chote hiki hatujawahi kupata udhamini ambao umekidhi mahitaji yote ya timu kama huu wa TBL,” alisema Tenga kwenye mkutano na waandishi uliofanyika kwenye ofisi za TFF.
“Lakini katika mwaka mmoja uliopita (tangu TBL ianze kudhamini) hatujawahi kushindwa kuisafirisha timu; kushindwa kulipa posho za wachezaji; kutanguliza watu wetu kwenda nje kuiandalia timu sehemu nzuri; kuzilipia tiketi za ndege timu tunazocheza nazo mechi za kirafiki na hata kuzilipia ada ya kucheza mechi (appearance fee).
“Posho za wachezaji zimepanda kwa karibu mara mbili na ndio maana leo wachezaji wanaijali timu yao. Yote haya ni kutokana na udhamini huu. Watu wanasema usione vinaelea….”
Tenga alisema kuwa udhamini huo ndio sasa umeanza kuzaa matunda na timu inafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na maandalizi ya muda mrefu.
“Sasa tunawaomba Watanzania waiombee timu na tunawashukuru wale waliokwenda Morocco kuishangilia kwa kuwa vijana wetu wanapata nguvu pale wanapoona kuna watu wako nyuma yao,” alisema Tenga.
Rais huyo wa TFF pia alisifu kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuiita timu Ikulu na kuongea na kula na wachezaji, akisema kitendo hicho kitasaidia kuongeza hamasa kwenye timu.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema kampuni yake itaendelea kuwa bega kwa bega na TFF na kwamba uhusiano baina ya pande hizo mbili umeimarika na utaendelea kuimarika.
Katika mkutano huo, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilikabidhi fulana maalum kwa ajili ya mashabiki ambao wamekwenda Morocco kuishangilia timu.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu alisema tayari fulana 250 zimegawiwa kwa mashabiki walioko Morocco na nyingine zilitarajiwa kusafirishwa jana.

No comments: