Thursday, August 15, 2013

YANGA NA AZAM JUMAMOSI TAIFA VIINGILIO 'VYA KUFA MTU'


Na Boniface Wambura, IMEWEKWA AGOSTI 15, 2013 SAA 6:34 MCHANA
KIINGILIO cha chini katika mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga na washindi wa pili, Azam FC kuashiria uzinduzi wa msimu mpya wa 2013/2014 kinatarajiwa kuwa Sh. 7,000.
Kiingilio hicho ni ongezeko la Sh. 2,000 kutoka kiingilio cha chini katika mchezo wa kufunga dimba la Ligi Kuu msimu uliopita, kati ya Simba na Yanga.  
Mara ya mwisho; Beki wa Azam, Joackins Atudo kushoto dhidi ya mshambuliaji wa Yanga SC, Hamisi Kiiza katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu, ambayo Yanga ilishinda 1-0. Mambo yatakuwaje Jumamosi Taifa?

Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa kivutio kwa wapenzi wa mpira wa miguu nchini itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni ambapo mshindi atakabidhiwa Ngao.
Iwapo dakika 90 za mechi hiyo hazitatoa mshindi, timu hizo zitatenganishwa kwa mikwaju ya penalti huku asilimia 10 ya mapato ya mechi hiyo yakienda kwa kituo cha kulelea watoto cha SOS.
Kiingilio cha Sh. 7,000 ni kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa itakuwa Sh. 10,000, VIP C Sh. 15,000, VIP B Sh. 20,000 na VIP A Sh. 30,000.
Wakati huo huo: Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoshirikisha timu 24 zilizogawanywa katika makundi matatu msimu huu (2013/2014) itaanza kutimua vumbi Septemba 14 mwaka huu.
Kila timu itakayoongoza kundi lake katika ligi itakayochezwa kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini) ndiyo itakayopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2014/2015.
Mechi za ufunguzi kwa kundi A zitakuwa kati ya Tessema vs Green Warriors (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam) wakati Septemba 15 mwaka huu ni Transit Camp vs Polisi Dar (Uwanja wa Mabatini, Pwani), Ndanda vs Friends Rangers (Uwanja wa Nangwanda, Mtwara) wakati Villa Squad vs African Lyon itachezwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Kundi B ni Burkina Faso vs Polisi Moro (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Mkamba Rangers vs Lipuli (Uwanja wa CCM Mkamba, Morogoro), Majimaji vs Mlale JKT (Uwanja wa Majimaji, Songea) wakati Septemba 15 mwaka huu Kimondo SC vs Kurugenzi (Uwanja wa Sokoine, Mbeya).
Mechi za ufunguzi kundi C ni Polisi Mara vs Polisi Dodoma (Uwanja wa Karume, Musoma), Kanembwa JKT vs Polisi Tabora (Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma), Stand United vs Mwadui (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), na Pamba vs Toto Africans (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza).
Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Oktoba 26 mwaka huu wakati wa pili utamalizika Machi 22 mwakani. 

No comments: