Wednesday, August 21, 2013

HATI ZA KUMILIKI ARDHI ZITOLEWE UPYA, ZA DIJITALI NA ZIHUSISHWE NA NAMBA YA MLIPA KODI (TIN)


Kamati ya Hesabu za Serikali imekutana na Wizara ya Ardhi kwa madhumuni ya kupitia Hesabu za Wizara kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2012.

 Changamoto za Wizara ni nyingi sana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amehoji mambo mengi sana na mengi ni wizi, upotevu wa mapato ya Serikali na malalamiko ya wananchi kuhusu ardhi. 

 CAG alitoa hoja za ukaguzi maeneo ya mapato kutokusanywa, kulimbikizwa na hata kukusanywa bila kuyawasilisha Wizarani.
 
Katika Mwaka wa Fedha 2011/12 Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni tisini na tisa (99 bilioni) lakini ilikusanya shilingi bilioni ishirini tu (20 bilioni) sawa na asilimia 21 ya makadirio.
 
CAG pia alihoji masuala ya viwanja vilivyopimwa, kugawiwa watu lakini watu hawakupewa hati ambapo zaidi ya viwanja 7, 342 vilikutwa ni viwanja vyenye shaka. Pia viwanja 160 jijini Dar es Salaam vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 555.8 milioni viligundulika ni viwanja ambavyo walijigawiwa maafisa wa Ardhi maana haoakuwa na ushahidi wowote wa mauzo ya viwanja hivyo. Hoja nyingine ni pamoja na ukiukaji wa sheria kwa kujengwa kwenye fukwe nk.
 
Katika Ripoti ya Hesabu za Serikali Kuu 2011/12 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alipendekeza kuanzishwa kwa haraka mfumo fungamanifu wa Taarifa za Ardhi, kutunza kumbukumbu kielektroniki na kuunganisha kuanzisha utaratibu wa kwamba wakati wa kusajili hati ya ardhi anayesajili kuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN).
 
Baada ya mjadala wa kina na kushauriana na wakaguzi na wataalamu Kamati ya Hesabu za Serikali iliona kuwa kuna haja kubwa sana ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo mzima wa kutoa hati za kumiliki Ardhi. 

Hivyo Uamuzi mkubwa tuliochukua ni kuagiza kuwa hati zote za kumiliki ardhi zitolewe upya, ziwe za dijitali na hati ziendane na namba ya Mlipa kodi (TIN). 
 
Kamati imeagiza kuwa  Wizara kutoa majibu ya utekelezaji wa agizo hilo ifikapo Mwezi Januari mwaka 2014. Tunaamini kuwa iwapo hati zote za ardhi zitakuwa za dijitali, tutaondoa kabisa tatizo la hati mbili kwenye kiwanja au shamba moja, itakuwa ni rahisi kwa usimamizi wa ardhi na itaondoa mgogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Pia tunadhani pia itakuwa rahisi kujua nani anamiliki ardhi kiasi gani, wapi nk. 
 
Tunaamini kuwa mfumo wa dijitali katika hati za ardhi utaongeza usalama zaidi kwa wamiliki wadogo wa ardhi na kuondokana kabisa au kwa kiasi kikubwa na hati za bandia ambazo zinaumiza zaidi wananchi masikini wanaotapeliwa kila wakati. Ardhi yenye hati za kidijitali na zinazotunzwa kielektroniki zitakuwa na thamani zaidi na zitawezesha mahitaji zaidi ya hati hizo kwa shughuli mbalimbali za wananchi.
 
Mapato yatokanayo na umiliki yatakusanywa kirahisi sana na kwa kuwa kila hati itakuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN)  itakuwa ni njia rahisi ya kuzuia ukwepaji kodi ya ardhi.  Kwa kuwa kamati imeagiza kuanza kutumika kwa risiti za elektroniki kwa malipo ya serikali, tutaweza kupandisha mapato ya Serikali na hasa kwenye halmashauri za wilaya na kuepukana na kodi sumbufu kwa wananchi.
 
Changamoto kubwa ni kama matajiri wenye ardhi kubwa watakubali mageuzi haya kwani hawapendi ijulikane kiwango cha ardhi wanachomiliki na pia itazuia ukwepaji kodi na kupunguza rushwa kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi. 
 
Mfumo huu hata hivyo uwezeshe watu kuweza kutafuta kwenye mtandao hati, iwe rahisi kutafanya utafutaji. Pia mfumo huu unaweza kusaidia sana suala la fidia kwa wananchi wanaohamishwa kupisha uwekezaji mkubwa kama kwenye sekta za madini na gesi asilia. 

Kwa mfano mwekezaji atapaswa kuhakikisha hati za kijiditali zinapatikana kwa wananchi wanaohamishwa kupisha mradi baada ya maridhiano ya wananchi hao kuhusu kupisha mradi na mahala watakapohamia.

Kuna haja pia hata hati za madini (mining rights) na leseni mbalimbali ziwe za dijitali na kuhusishwa na TIN. Huko ndipo tunapaswa kuelekea.
 
Zitto Kabwe
MwenyeKiti PAC  
Agosti 21, 2013 - Dar es Salaam

WANARIADHA WAANZA KUIPA MEDALI POLISI TANZANIA NCHINI NAMIBIA

 Mshindi wa kwanza katika mbio za mita 10000 kwa Wanaume Fabian Nelson (Tanzania) katika Michezo ya Umoja wa wakuu wa Polisi kwa Nchi za kusini mwa Afrika  (SARPPCO) Nchini Nambia  akishangilia na bendera ya taifa mara baada ya kumaliza mbio hizo katika uwanja wa taifa wa Namibia (Picha zote na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Windhoek Namibia)
 Mshindi wa kwanza katika mbio za mita 10000 kwa Wanaume Fabian Nelson (Tanzania) akivalishwa medali ya dhahabu na mmoja wa makamishna wa Polisi wa Namibia katika Michezo ya Umoja wa wakuu wa Polisi kwa Nchi za kusini mwa Afrika  (SARPPCO) katika uwanja wa taifa wa Namibia.
 Baadhi ya wanamichezo wa Tanzania wakishangilia ushindi wa kwanza katika mbio za mita 10000 kwa Wanaume katika Michezo ya Umoja wa wakuu wa Polisi kwa Nchi za kusini mwa Afrika  (SARPPCO) katika uwanja wa taifa wa Namibia. 
Wanaridaha  wa mbio za mita 10000 kwa Wanaume wakikimbia katika Michezo ya Umoja wa wakuu wa Polisi kwa Nchi za kusini mwa Afrika  (SARPPCO) Nchini Nambia.

Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi,Windhoek
Wanariadha wanaowakilisha Jeshi la Polisi Tanzania katika michezo ya Umoja wa wakuu wa Polisi kusini mwa Afrika SARPCCO nchini Namibia wameanza vyema mbio hizo baada ya kufanikiwa kunyakua medali za Dhahabu na fedha katika mbio za mita elfu 10000 wanaume.

Aliyenyakua medali ya dhahabu ni Mwanariadha Fabian Nelson ambaye alitumia dakika 30 na sekunde 42 huku akifuatiwa na Wilbrado Peter (Tanzania) ambaye alitumia dakika 30 na sekunde 45 na kuwaacha wanariadha wengine nyuma kutoka mataifa ya Zimbabwe,Namibia,Botwasana na Angola.

Wengine walioipatia Tanzania Medali ni pamoja na Basili John  mita 800 (Shaba ) na Mohamed Ibrahim mchezo wa kurusha kisahani (shaba).

Katika mpira wa miguu mechi ya ufunguzi ilizikutanisha wenyeji Namibia na Msumbiji ambapo Namibia iliichapa Msumbiji mabao 2 kwa 0 huku kwenye mpira wa miguu wanawake Namibia na Angola zilitoka suluhu ya bila kufungana.

Tanzania itaanza kutupa karata yake katika mpira wa miguu dhidi ya Zambia ambapo Tanzania imepangwa kundi B ikiwa na timu za Zambia, Angola ,DRC na Lesotho huku Kundi B lina timu za Namibia, Msumbiji, Botswana na Zimbabwe.

KATUNI YA LEO

SAHRINGON yazifunda Asasi za Kiraia Tanzania

Na Salum Mkandemba
MRATIBU Taifa wa Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRINGON Tanzania), Martina Kabisama, amezitaka Asasi za Kiraia nchini kusaidia Watanzania katika mchakato wa Katiba unaoendelea ili kuepuka matakwa ya wanasiasa kugubika mchakato huo.

Martina alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akichangia mada katika Mkutano wa Asasi za Kiraia za Afrika Mashariki (EACSO), ulioratibiwa na Chama cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania (TANGO), kujadili mambo kadhaa, ikiwamo Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa, katika Mkutano Mkuu wa Global Social World wa mwaka 2011, pamoja na mambo mengi, Afrika ilishauriwa kuwa na Asasi za Kiraia zinazoshiriki kwa mapana kuwasaidia wananchi katika michakato ya katiba na sio kukurupukia matakwa ya watawala wa nchi.

“Asasi za Kiraia Tanzania zinapaswa kujifunza kutoka kwa asasi kama hizo za Kenya katika kuwezesha upatikanaji wa katiba inayomtambua na kumthamini Mtanzania masikini, sio kuegemea katika malumbano ya kujadili hatima ya Muungano na kusahau mambo muhimu,” alisema Martina.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Dira Afrika Mashariki (Vision East Africa Forum), Dk Azaveli Lwaitama, alizitaka Asasi za Kiraia nchini kutohofia tofauti ya kiuchumi baina ya nchini za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani zina nafasi sawa katika kunyanyua maendeleo ya nchi hizo.

Dk Lwaitama alibainisha kuwa, moja ya changamoto inayoikabili Jumuiya ya Afrika Mashariki ni tofauti ya kiuchumi baina ya mataifa na watu wake, ambayo imo hata miongoni mwa wananchi wa nchi moja, hivyo Asasi za Kiraia zinapaswa kuwaongoza Watanzania kujifunza kutoka kwa wenzao.

“Tofauti ya kiuchumi ipo, lakini Watanzania hatupaswi kuihofia, badala yake Asasi za Kiraia zisimame katika kufanikisha kuwapo kwa mchakato wa Katiba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ili kuwawezesha Wanajumuiya kunufaika ipasavyo,” alisisitiza Dk Lwaitama.
Aliongeza kuwa, Katiba ya Jumuiya hiyo, itasaidia uharaka wa maendeleo kwa nchi wanachama, kupitia uwekezaji wa pamoja utakaofanikisha kurejea kwa Mamlaka za Usafiri Majini, Sarafu ya Pamoja na Mashirika ya Reli na Ndege ya Afrika Mashariki.

RAIS ATUNUKU HATI IDHINI KWA VYUO NANE NCHINI

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa Vyuo Vikuu mara baada ya kuwatunuku hati Idhini Ikulu jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Habari Mseto Blog) 

Na Immaculate  Makilika- Maelezo
 
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ametunuku hati Idhini kwa vyuo vikuu na vyuo vishiriki 8 baada ya vyuo hivyo kutimiza taratibu zote za uanzishwaji wake hapa nchini.

Vyuo vilivyotunukiwa hati  baada ya kutimiza taratibu zote ni Chuo Kikuu cha Tumaini(TUMA),Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT),Chuo  Kikuu Kishiriki  cha Ruaha(RUCo),Chuo Kikuu  cha Mount Meru(MMU),pamoja na Chuo Kikuu cha Arusha(UoA).

Vyuo vingine vilivyotunukiwa hati hiyo ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es salaam(TUDARCo) ,Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi  na Teknolojia Arusha (NM-AIST) na Chuo Kikuu cha Sayansi  na Teknolojia Mbeya(MUST).

Rais  Kikwete  alivitunuku  vyuo hivyo kwenye hafla fupi iliyofanyika  leo Ikulu jijini  Dar es Salaam , ambapo  alisema  vimepiga hatua kubwa ya  kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiandikisha hadi kufikia  laki moja sitini na sita elfu mwaka 2013 ,ukilinganisha na idadi ya wanafunzi elfu arobaini ya mwaka 2005.

 “Idadi kubwa ya wanafunzi pekee haitoshi,ubora wa elimu uzingatiwe . Ikiwemo kupata wakufunzi wengi na wenye sifa  ni lazima sisi wenyewe tuwekeze ndani ili kupata wakufunzi wakutosha katika vyuo vyetu ,” alisema Rais Kikwete.

Aidha Rais  Kikwete  alivitaka vyuo hivyo kutekeleza  mkakati wa elimu wa  Matokeo  Makubwa Sasa (Big results now) ipasavyo  ili kuboresha elimu nchini kwa kuimarisha miundombinu  ya  vyuo vikuu nchini.

Aliongeza kuwa  lazima viwe na mahitaji yote muhimu kwa kutoa elimu bora ikiwemo vifaa vya kutosha,maabara,vyuo vya zamani viwekwe kwenye viwango  ili kukidhi utoaji wa elimu bora, na kusisitiza vyuo vikuu vyetu vishirikiane na vyuo vikuu vya nje na kuvishauri   vitafute vyanzo vingine vya mapato ili  kukidhi uendeshaji badala ya kutegemea ada.

 Utoaji wa hati Idhini kwa vyuo vikuu  ni zoezi endelevu linalolenga  kuboresha  kiwango cha utoaji elimu  ya juu nchini  ili kuwezesha wahitimu  kukabiliana na changamoto  za maendeleo  ya taifa letu kwa ujumla. Kwa mara ya mwisho zoezi hili lilifanyika  tarehe 18 Agosti,2010 ambapo jumla ya vyuo vikuu na vyuo vishiriki  13 vilitunukiwa hati Idhini.

24 WAITWA TAIFA STARS KUIVAA GAMBIA

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameita kambini wachezaji 24 kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu nchini humo.
Wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini Agosti 29 mwaka huu kabla ya saa 1 kamili usiku. Kambi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kwenye hoteli ya Accommondia jijini Dar es Salaam.
Makipa walioitwa katika timu hiyo Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na David Luhende (Yanga).
Viungo Khamis Mcha (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Dilunga (Ruvu Shooting), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Amir Kiemba (Simba), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga), John Boko (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na Juma Liuzio (Mtibwa Sugar).
RAMBIRAMBI MSIBA WA BARAKA KITENGE
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Yanga na Taifa Stars, Baraka Kitenge (74) kilichotokea leo mchana (Agosti 20 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Kitenge akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
Kitenge amefia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo alikuwa amelazwa akisumbuliwa na kansa ya uti wa mgongo. Enzi zake katika Yanga na Taifa Stas alicheza na wachezaji kama akina Athuman Kilambo na Abdulrahman Juma.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kitenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Yanga na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwa Marehemu, Yombo Vituka (Jet) jijini Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Kitenge mahali pema peponi. Amina
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Rasimu ya Katiba; Dk. Slaa awageukia Viongozi wa Dini

Wanafunzi wakiishangaa helkopta ya Dk. Wilbroad Slaa ikishuka katika Uwanja wa Wajenzi Dodoma.

Na Bryceson Mathias, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, jana Juni 19, 2013 katika viwanja vya Wajennzi Dodoma, amewageukia Viongozi wa Dini nchini akiwataka wakiwa Madhabahuni na kugeukia Kibra, wajikite kuhubiri Haki ya Watanzania.
Mbali ya usia huo, Dk. Slaa pia aliwauliza wananchi wa Dodoma Swali Gumu iwapo Vyama na wao nani alianza kuwepo mkoani Dodoma, Je ni Vyama au Wananchi? Wakajibu wao, akaonya TANU, UNIP,vilikuwepo vikafa; hivyo wasikubali kuburuzwa na Vyama.
Akizungumzia Rasimu ya Katiba baada ya Mwanasheria wa Chadema Edson Mbogolo kutoa Elimu ya Mabadiliko ya Katiba yanayoungwa Mkono na Chadema na yale yanayokataliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), ambapo Slaa alishangaa nchi kuwa na Amiri Jeshi Wakuu Wawili.
“Hakuna Mtanzania asiyemfahamu Jaji Joseph Sinde Warioba, ni Jaji na alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alimwamini akamchagua awe Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya. Leo ametoa mapendekezo CCM ajabu wanayapinga.
“Wapinzani tunaaminika tunapinga kila Kitu, ila mapendekezo ya Jaji Warioba tumeyakubali asilimia kubwa kwa sababu inaeleza mustakabali Uchumi wa Taifa na Rasilimali za Vizazi Vyetu, Tunu za Taifa, Malengo Makuu, Uwazi, Utu, nauliza, CCM na Chadema nani Mpinzani?”..wananchi CCM!.
Slaa alisema, Rasimu imeeleza Serikali ilinde Amani Uchumi iondoe Umaskini, Izuie Vitisho, Ubaguzi, Rushwa,Uonevu, Dhuluma,Unyanyasaji na Utajiri utumike kwa wote na mengi mengine, lakini CCM inapinga yote hayo, Je Chadema na wo nani anamtetea Mwananchi?
“Twiga wanasafirishwa kwenye ndege, Meno ya Tembo kwenye Meli tena za Viongozi wa CCM walinzi wa Usalama wote wa ndani na Mipakani wapo, hoja ya kuwadhibiti waharifu hao inapingwa, si wanataka wakifanya hivyo sheria isiwakamate?”.alisema Slaa na kushangiliwa.
Aidha wananchi walitoa maoni ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa wakuu wa wilaya na Mikoa, wanaolipwa Mil.11/-, Rais ashitakiwe anapofanya makosa, Wawekezaji wawekeze kwa masharti ya Watanzania, Tume huru, IGP, Spika asitokane na Chama, Mawaziri wasiwe Wabunge, IGP athibitishwe na Bunge, na kwamba gharama za Serikali Tatu ni ndogo.

CHADEMA yamtaka Waziri Makala asikumbatie watuhumiwa wa Ufisadi

Na Bryceson Mathias, Mvomero
DIWANi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kata ya Nyandira  wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, amemtaka Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala, asiwakumbatie watuhumiwa wa Ufisadi wa zaidi ya Mil. 10/- za Minara ya Simu ya kijiji hicho.
Diwani wa CHADEMA kata hiyo, Peter Zengwe amesema Makala amepokea kuwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wa chama hicho wilaya, wamewapokea aliyekuwa Mwenyekiti, Yodosi Msimbe, na aliyekuwa Mtendaji Elnestina Mponda.
 Zengwe alitoa Kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Makala uliofanyika katika kijiji cha Nyandira Augosti 19, na kuhutubiwa na Naibu Waziri huyo.
,”Makala katika hali iliyowashangaza wananchi, aliwapokea kiwepesi sana watuhumiwa hao kuwa wanachama wa CCM, ilihali anajua Chadema kimekuwa kikirumbana nao baada ya kuwabaini kuhusika na tuhuma hizo na kuwashitaki Polisi toka 2008.
“Kwa kuogopa Ukali wa Chadema, watuhumiwa hao wameona wakimbilie CCM maana huko ndiko kunakowafuga watuhumiwa na kuwakumbatia, maana Wimbo wa Chadema M4C, hawauwezi ”. Alisema Zengwe.
Katika mkutano huo, Makala aliongozana na Mhandisi wa Wilaya aliyejulikana kwa jina Moja la Jacob, ambaye imedaiwa alikwenda kwa lengo la kutoa amri ili Jengo la Chadema lililojengwa na Zengwe, zilizvunjwe, madai limejengwa chini ya kiwango, jambo ambalo alikanusha..
Awali wanachama hao walitangaza kujiunga na Chadema,lakini baada ya kubanwa ili watoe maelezo kuhusiana na tuhuma zinazowakabiri, waliamua kurejea CCM waliokotoka, na waziri Makala kuwapokea kwenye mkutano huo

NSSF YAZINDUA KAMPENI YA MALARIA

 Balozi wa Malaria ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodger Tenga akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupiga vita ugonjwa wa malaria iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya maofisa wa NSSF wakiwa katika uzinduzi huo.  
 Baadhi ya wadau waliohudhuria hafla hiyo.
 Baadhi ya maofisa wa NSSF wakiwa katika uzinduzi huo.  
 Balozi wa Malaria ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodger Tenga akipeana mkono na Meneja Kiongozi, Uhusiano Huduma kwa Wateja wa NSSF, Eunice Chiume wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupiga vita ugonjwa wa malaria iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
 Meneja wa Mafao ya Matibabu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ali Mtulia akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kupiga vita ugonjwa wa malaria kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na NSSF.

No comments: