Shahidi wa tano katika kesi ya kutorosha wanafunzi inayomkabili
Mchungaji wa Kanisa la TAG, raia wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo
(DRC), Jean Felix Bamana ameieleza mahakama namna alivyolazimishwa
kufanya mapenzi na mchungaji huyo.
Shahidi huyo, Angela Swai (19), akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu,
Naomi Mwerinde wa Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi, alisema Mchungaji huyo
alimlazimisha kufanya kitendo hicho jaribio ambalo lilishindikana
kutokana na mshitakiwa huyo kukataa kutumia kondomu.
Akiongozwa na mwendesha mashtaka, wakili wa serikali, Esther Majaliwa,
katika ushahidi wake, Shahidi huyo alieleza Mahakama hiyo alivyokutana
na mshtakiwa kwa mara ya kwanza na mara ya pili ambapo alisema alikutana
naye kupitia marehemu mama yake mzazi huku mara ya pili akikutana naye
kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Shahidi huyo alieleza mahakamani hapo kuwa alikutana na mshtakiwa kwa
mara ya kwanza kupitia mama yake na alimtambulisha yeye na ndogo wake
aliyemtaja kwa jina la Arthur kuwa mchungaji huyo ni baba yao mwingine
na waliendelea kufahamiana kwani alikuwa ni rafiki mkubwa wa mama na
mshirika wake katika Biashara ya Madini.
Alisema kwa kipindi kirefu hakuwahi kumuona hadi alipokutana naye kwa
mara ya pili mwaka jana kupitia mtandao wa Facebook ambapo alimwomba
urafiki kwa nia njema kwani alikuwa ni rafiki mkubwa wa marehemu mama
yake, na kuongeza kuwa mawasiliano yalikuwa ni ya kawaida tu.
Shahidi huyo alisema baada ya hapo mshtakiwa alianza kumsisitiza kuhamia
Dar es Salaam kwa ahadi ya kumsaidia kuendelea na masomo baada ya
kumueleza amefukuzwa shule jambo ambalo yeye binafsi alilikataa.
Alisema baada ya kukataa kukubaliana na wazo la kwenda Dar es Salaam,
mshtakiwa huyo alimwambia atafika Moshi ambapo alifikia katika Hoteli ya
Moshi View, Februari 14, mwaka huu na kufanya naye mawasiliano kupitia
simu ya mdogo wake aliyetajwa mahakamani hapo kwa jina la Arthur Swai,
akimtaka kumfuata hotelini hapo.
Shahidi huyo alieleza Mahakama ya Hakimu Mwerinde kuwa Mawasiliano kati
yake na mshtakiwa yaliendelea ambapo katika kipindi hicho mshtakiwa
alikuwa akimsisitiza aende Dar es Salaam na ikiwezekana waondoke wote,
jambo ambalo hakukubaliana nalo.
Kutokana na kutokubaliana na matakwa ya mshtakiwa, shahidi huyo namba
tano katika kesi hiyo ya makosa ya Jinai, alisema ushawishi ulihamia kwa
mdogo wake na kuanza kumtaka mdogo wake amshawishi akubali kuhamia Dar
es Salaam akiahidi kumnunulia simu pamoja na kuwapeleka Ulaya.
Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa, jana ilishuhudia upande wa mashtaka
ukipandisha mashahidi watatu, Mkuu wa Shule ya Sekondari MaryGoreti,
Sister Lucresia Njau, dereva teksi Yusuph Khamisi ambao ni shahidi namba
tatu na namba nne na Angel Swai ambaye alikuwa shahidi wa tano.
Kesi hiyo itasikilizwa tena mahakamani hapo Agosti 23, mwaka huu ambapo
upande wa mashtaka umeahidi kuwasilisha mahakamani hapo mashahidi
wengine watatu.
No comments:
Post a Comment