Tuesday, July 9, 2013

KIJANA AJILIPUA KWA MAFUTA YA PETROLI MJINI DODOMA, KISA WIVU WA MAPENZI


Picha na Maktaba ya Sufianimafoto.
Na Mwandishi Wetu, DODOMA, Tanzania
Mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) cha mkoani Dodoma, aliyejulikana kwa jina la Taliki Juma (22), amedaiwa kujiua kwa staili ya kujilipua kwa mafuta ya Petroli hadi kufa kwa kisa cha mapenzi. 

Taarifa zilizoufikia mtandao huu, zinasema kuwa katika tukio hilo ulizuka moto mkali jambo lililosababisha watu wengine wanane kujeruhiwa na moto huo. 

Tukio hilo limethibibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, aliyeeleza kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 12:30 jioni katika Kitongoji cha Machaka Kata ya Nzughuni mkoani humo. 

Aidha Kamanda huyo alifafanua kwamba, awali mwanafunzi huyo, alionekana akitoka katika Kituo cha kuuzia mafuta cha Nane Nane, huku akiwa amenunua mafuta ya Petroli Lita tano, na kwenda nayo hadi katika Saluni moja ya Irene Mapunda, anayesadikiwa kuwa ndiye aliyekuwa mpenzi wake, na kisha kujimwagia na kujiwasha moto. 

Wakielezea tukio hilo baadhi ya mashuhuda waliokuwa karibu, walisema kuwa baadhi ya watu walipomuona akianza kujimwagia mafuta hayo walijaribu kumsihi na kumshika ili asijilipue lakini aliwashinda nguvu na kuingia ndani ya Saluni hiyo na kuwasha kiberiti na kusababisha moto mkubwa kuwaka na kuwajeruhi watu waliokuwamo na kuteketeza mali zote zilizokuwa katika Saluni hiyo. 

 ''Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kumapenzi, hata hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma bado linaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hili'' alisema Kamanda Misime.

No comments: