Monday, July 29, 2013

Chuo cha Taifa cha Ulinzi chatoa wahitimu wa kwanza • Serikali yaahidi kukisaidia kuwa kitovu cha taaluma


Julai 20, 2013 imeshuhudia Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Kunduchi Dar es Salaam kikitoa wahitimu wake wa kwanza katika Mikakati ya Ulinzi na Usalama wa Taifa tangu JWTZ kuanzishwa.
Kozi hiyo ya kwanza ya aina yake nchini iliyojumuisha jumla ya Maafisa wakuu 20, kati yao nane (8) kutoka JWTZ ilifungwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal.
Wahitimu wengine waliosalia walitokea Taasisi mbali mbali za Serikali zikiwemo Ofisi ya Rais (Maafisa watatu), Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Maafisa wawili), Jeshi la Polisi (Maafisa wawili), Afisa mmoja mmoja kutoka Wizara ya Ulinzi na JKT, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, PCCB na Jeshi la Magereza.
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kozi hiyo wanafunzi walijifunza Utengenezaji wa sera na mikakati; Usalama, migogoro na vita; Mahusiano ya kimataifa; Siasa jamii; Uchumi; Kilimo na viwanda; Mazingira ya usalama kimataifa; Matukio duniani; Majirani wa karibu na wa kimkakati wa Tanzania na Mikakati na muundo wa usalama wa Taifa.
Akifunga kozi hiyo, Makamu wa Rais wa Kamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal aliwataka wahitimu kuendelea kuwa wanafunzi wema wa chuo hicho hata baada ya kuhitimu kwani elimu haina mwisho. Aliwataka kutunza sifa njema ya chuo mara watakaporejea sehemu zao za kazi.
Makamu wa Rais alisema kuwa Mahafali hayo yamekuja wakati ambapo kuna mazingira tata ya kiusalama kimataifa na ndani ya nchi. “Matukio ya hivi karibuni ya vurugu mkoani Mtwara na ulipuaji mabomu mkoani Arusha hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania. Hivyo sifa yetu njema ya kuwa kituo cha amani imeguswa na watu wasioitakia mema nchi yetu”, alikiri Dkt. Bilal.
Alibainisha pia kuwa nchi yetu pia inakabiliwa na tishio kubwa la kiusalama kutokana na migogoro ya usimamizi wa maliasili kama vile madini, gesi, ardhi na maji. Migogoro hii inahitaji viongozi wenye uwezo wa kufanya tathmini mwanana katika masuala hayo na kuchukua hatua madhubuti za kimkakati. “Ni imani yangu Chuo hiki kitaendelea kuwapa nyenzo wanafunzi wake zitakazoweza kuchanganua na kuchambua matatizo yaliyopo na kupendekeza namna ya kuyapatia ufumbuzi”, aliongeza Dkt. Bilal.
Akizungumzia changamoto ya kutofika kwa Maafisa walioalikwa kutoa mada kutoka wizara mbali mbali wakati wa kozi hiyo, Dkt. Bilal alimuagiza Waziri wa Ulinzi na JKT kushughulikia suala hilo na wadau mbali mbali kutoka wizara husika ili kupata ufumbuzi. 
Akihitimisha hotuba yake, Makamu wa Rais aliahidi kuwa Serikali itafanya kila linalowezekana kusaidia chuo hicho kufikia lengo lake la kuwa kitovu muhimu cha taaluma nchini. Aliiagiza Wizara ya Ulinzi na JKT ihakikishe kwamba idara za Serikali zinadhamini makada wao kupata mafunzo katika Chuo hicho na kuhakikisha kuwa nafasi za mafunzo zinatolewa kwa nchi marafiki.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na JKT, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na JKT, Bw. Job Masima alimpongeza Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange kwa kusukuma wazo la Tanzania kuwa na Chuo chake kikuu cha Ulinzi wa Taifa. Alimshukuru pia Mkuu wa Chuo hicho, Luteni Jenerali Charles Lawrence Makakala kwa kuongoza kwa weledi mkubwa mchakato mzima wa kuandaa na kuusimamia mtaala wa chuo hicho.
Mapema akitoa hotuba yake kabla ya kutunuku heshima ya kuhitimu “ndc” kwa wahitimu, Mkuu wa Chuo hicho, Luteni Jenerali Makakala aliwatambua watoa mada wafuatao kwa mchango wao wa kufanikisha kozi hiyo: Marehemu Meja Jenerali Anatory Kamazima, Meja Jenerali (Mstaafu) Herman Lupogo, Mhe. Bernard Membe (Mb) na Meja Jenerali (Dkt) Charles Muzanila.
Wengine ni Prof. Daudi Mukangara, Prof. Elisante Ole Gabriel, Prof. Eginald Mihanjo, Prof. Issa Shivji, Prof. Mohabe Nyirabu, Prof. Rwekaza Mukandala, Prof. Severine Rugumamu, Prof. Ibrahim Lipumba, Dkt. Edward Hosea, Dkt. Benson Bana na Dkt. Reginald Mengi.
Mahafali ya kuhitimu kwa kozi hiyo ya kwanza ya Chuo hicho yalihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Pandu Kificho, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi, Mhe. Anna Abdallah, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Spika Mstaafu Pius Msekwa, Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange, Wakuu wa Majeshi Wastaafu Jenerali Hagai Mrisho Sarakikya na Jenerali George Waitara, Mabalozi, Maafisa, Askari, vyombo vya habari na wananchi mbali mbali.
Kozi hiyo ya Kwanza ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi ilianza rasmi tarehe 3 Septemba, 2012 na kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 10 Septemba, 2012. Kauli Mbiu ya Chuo hicho ni Kusaka Uhuru, Busara na Amani.

No comments: