Viongozi
saba wa Jumuiya ya Uamsho wamepunguziwa masharti ya dhamana na Mahakama
ya Wilaya ya Mwanakwerekwe, huku watumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar wakishindwa kujitokeza kuwadhamini tangu dhamana ilipowekwa
wazi na Mahakama Novemba 4 mwaka huu.
Hatua ya kupunguziwa masharti ya dhamana,
imekuja baada ya wakili wa upande wa utetezi, Salum Tawfq na Abdallah
Juma kuomba masharti yaangaliwe upya kufuatia uwezo mdogo wa washitakiwa
na watumishi wa umma kuogopa kujitokeza kuwadhamini.
Alidai tangu dhamana hiyo kuwekwa wazi,
wateja wao wameshindwa kuyatekeleza kutokana na kipato cha Wazanzibari
kuwa kidogo, na washitakiwa kushindwa kumudu kuweka dhamana ya Shilingi
milioni moja kwa kila mshitakiwa na wadhamini wawili kwa kiwango kama
hicho.
Alidai sharti la kila mshitakiwa kuwa na
wadhamini watatu ambao ni watumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, nalo limekuwa ni kikwazo kwa wateja wao kutokana na kesi
yenyewe kuihusu Serikali dhidi ya Uamsho.
Alidai kwamba pamoja na Mahakama hiyo
kutaka uongozi wa chuo cha mafunzo, kuwapatia washitakiwa hao huduma
zote muhimu kama ambazo wanapatiwa mahabusu wengine, amri hiyo ya
mahakama bado haijatekelezwa, zaidi ya kupewa haki ya kubadilisha nguo
na kutonyolewa tena ndevu kama awali.
"Tunashukuru angalau wamepewa fursa ya
kubadilisha nguo na hawajanyolewa tena ndevu, lakini bado wananyimwa
fursa za kukutana na ndugu na jamaa zao, fursa ya kusoma Qur'an tukufu
na kushiriki ibada ya pamoja ya sala ya Ijumaa, pamoja na kufungiwa kila
mmoja katika selo yake kwa muda wa saa 24 tangu walipowekwa kizuizini,"
alidai Wakili huyo.
Alieleza kuwa vitendo hivyo vinakwenda
kinyume na sheria namba 7 kifungu cha 41 cha mwenendo wa makosa ya
jinai, juu ya haki ya washitakiwa kuwasiliana na mawakili wao na kupata
huduma za hospitali na mambo mengine wanapokuwa chini ya ulinzi au
uangalizi maalum.
Upande wa mwendesha mashitaka wa Serikali,
ukiongozwa na Ramadhan Abdallah na Amour Ame, ulidai hawana pingamizi
na washitakiwa kupunguziwa masharti ya dhamana kwa vile ni jukumu la
Mahakama lakini kama wahusika haki zao za kikatiba zimevunjwa, wana haki
ya kufungua kesi ya madai katika mahakama kuu.
Ramdhan alieleza kuwa kwa mujibu wa Ibara
ya 25 A (1), ya katiba ya Zanzibar, ya mwaka 1984 imetoa uhuru kwa mtu
yeyote kufungua shauri katika mahakama kuu iwapo ataona kuwa katiba
imevunjwa au inavunjwa au inaelekea kuvunjwa.
Hakimu Msaraka Ame Pinja alieleza
kukubaliana na hoja ya kupunguza masharti ya dhamana na kutaka kila
mshitakiwa kuweka dhamana ya fedha taslimu Sh. 500,000 na wadhamini
wawili kwa kiwango kama hicho, kuwasilisha hati ya kusafiria au
kitambulisho cha Mzanzibari mkazi na wadhaminiwe na watumishi wawili
badala ya watatu ambao lazima wawe ni wafanyakazi wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi waliofikishwa Mahakamani hapo ni
pamoja na Amir Farid Hadi Ahmed, Sheikh Mselem Ali Mselem, Sheikh Azzan
Khalid Hamdan, Sheikh Mussa Juma Issa, Sheikh Suleiman Juma Suleiman,
Sheikh Khamis Ali Suleiman na Sheikh Hassan Bakari Suleiman na kama
ilivyo ada walifikishwa chini ya ulinzi mkali.
CHANZO:
NIPASHE
Watatu waachiwa huru sakata la kusafirisha nje wanyama hai
Mkurugenzi
wa Mashtaka nchini (DPP) amewaondolea mashtaka washtakiwa watatu katika
kesi ya uhujumu uchumi, kula njama na kusafirisha na kuuza nje ya nchi
wanyama 136.
Washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na
tuhuma ya kuuza nje ya nchi wanyama hao aina 14 tofauti ambao ni nyara
zenye thamani ya Dola za Marekani 113,715.00 sawa na Sh. 170,572,500.00,
mali ya serikali ya Tanzania.
Hata hivyo, pamoja na kufuta mashtaka
dhidi ya watuhumiwa hao, DPP ametoa kibali cha kuunganishwa kwenye kesi
hiyo mtu mwingine, Michael Mrutu (30) ambaye ni afisa usalama wa kampuni
inayosimamia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ya
Development Company Limited (KADCO).
Wakili wa Serikali Arafa Msafiri
akisaidiana na Evetha Mushin na Pius Hila, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi, Simon Kobelo, walidai mahakamani hapo kuwa,
DPP amechukua uamuzi huo kwa mujibu wa sheria inayompa nguvu ya
kumwondolea mashtaka mtuhumiwa yoyote na kwamba Mrutu anakuwa mshatkiwa
wanne kwenye kesi hiyo.
Walioondolewa mashtaka ni Jane Mbogo
ambaye ni Mfanyakazi wa KIA raia wa Kenya, Veronica Beno Afisa Mkuu wa
usalama na Locken Kimaro ambaye ni Afisa Usalama wa kampuni hiyo.
Baada ya Mrutu kupandishwa kizimbani na
kuunganishwa katika kesi hiyo, aliiomba mahakama kumpa nafasi ya kuweka
wakili, ambapo wakili wa serikali alieleza mahakama hiyo kuwa uwezo wa
kutoa dhamana kwa mshtakiwa huyo haupo chini ya mahakama hiyo bali
Mahakama Kuu.
Hakimu Kobelo alisema mshtakiwa huyo
anapaswa kupeleka ombi Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata dhamana kutokana
na kwamba mahakama hiyo haina nguvu kisheria ya kusikiliza kesi hiyo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni
Mfanyabiashara Kamran Ahmed raia wa Pakstani na mkazi wa Arusha, Hawa
Mang’unyuka (51) mfanyabiashara na mkazi wa jijini Dar es Salaam, Martin
Kimati (58) ambaye alikuwa afisa mifugo mwajiriwa wa serikali na sasa
ni mfanyabiashara na mkazi wa Kibosho.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda makosa
hayo kabla na baada ya Novemba 26 mwaka 2010, kinyume na kifungu na 57
(1) na 60 cha sheria ya
uhujumu uchumi na kudhibiti uhalifu, ambapo wanyama hao walisafirishwa hadi mji wa Doha nchini Qatar.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment