Na Mwandishi wetu
Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) limesema kuwa Chuo Cha Agape hakina
Ithibati ya kukiwezesha kutoa mafunzo yoyote ya ngazi ya Stashahada,
hivyo hakiwatambui wanafunzi zaidi ya 33 wa ngazi hiyo waliohitimu
masomo yao chuoni hapo.
Akizungumza na NIPASHE j jijini Dar es
Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Primus Nkwera, alisema
kuwa, chuo hicho kilipata usajili wa awali kwa ajili ya kutoa mafunzo
ya ngazi ya cheti, wakati kikiendelea kufuata taratibu mbalimbali
kilichopewa na baraza hilo ili kiwe na sifa stahiki.
Dk. Nkwera alisema kuwa mbali na chuo
hicho kusajiliwa mwaka 2010, na kupewa maelekezo ya kufuata ili
kukamilisha taratibu za kupata sifa stahiki, lakini hakikufanya hivyo
badala yake kiliamua kutoa mafunzo ya ngazi ya Stashahada kwa
makubaliano na Chuo Cha Taifa Cha Biashara (CBE), jambo ambalo
halikubaliki kisheria.
Alisema kuwa alipata taarifa za kuwapo kwa
makubaliano kati ya vyuo hivyo viwili, na alipoamua kufuatilia
aligundua kuwa mkataba walioingia haupo kisheria kwani CBE haina uwezo
wala mamlaka ya kusajili chuo kingine.
“Ni kweli kuna taarifa za kuwapo kwa
mkataba wa makubaliano kati ya vyuo hivyo, niliukabidhi mkataba huo kwa
wataalam wa sheria ambao waliniambia kuwa mkataba huo ni batili,”
alisema Dk.Nkwera.
Aidha, Dk. Nkwera alisema atauandikia
uongozi wa CBE ili kuuonya kutokana na kukiuka utaratibu, na wakati huo
huo akisuburi taarifa ya wakaguzi wa baraza hilo waliokitembelea chuo
hicho hivi karibuni ili achukue hatua.
Akizungumzia malalamiko ya wanafunzi hao,
Dk. Nkwera, alisema kuwa ni vyema wakawasiliana na baraza hilo ili
kuangalia nini cha kufanya kuwawezesha watambuliwe na baraza hilo na
kuendelea na masono ya juu.
John Nzena, mwanafunzi aliyehitimu masomo
yake chuoni hapo mwaka huu, aliiambia NIPASHE kuwa alijiunga na chuo
hicho mwaka 2010 kwa kozi ya Stashahada ya Ugavi, lakini alipomaliza
mwaka huu na kuanza taratibu za kujiunga na elimu ya ngazi ya juu kwenye
vyuo vingine, aliambiwa kuwa chuo alichotoka hakitambuliki.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Dk.
Leonard Mbilinyi, alisema kuwa amepata malalamiko ya wanafunzi hao
kuhusiana na kukataliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, na kusema
anashangwazwa na kuwepo kwa taarifa ya kwamba hakuna mkataba wa
makubaliano yaliyofanywa kati ya chuo chake na CBE.
Dk. Mbilinyi alisisitiza kwamba mkataba
huo ni halali kwani ulishirikisha pande zote mbili, na kwamba nyaraka
zote anazo, kinachofanyika sasa ni mazungumzo kati yake yeye, CBE na
Nacte ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment