Monday, November 26, 2012

Vettel bingwa wa dunia mara 3


Mjerumani Sebastian Vettel, dereva wa timu ya magari ya Red Bull, aliibuka bingwa wa dunia, alipoweza kuwazidi madereva wenzake kwa pointi tatu katika mashindano ya Brazil ya langalanga siku ya Jumapili.
Sebastian Vettel
Dereva mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuwa bingwa wa dunia mara tatu mfululizo katika mashindano ya langalanga
Hii ni mara ya tatu mfululizo Vettel anaibuka bingwa wa dunia.
Katika mashindano yaliyojaa matukio mbalimbali, ikiwa pia ni pamoja na mvua, Vettel alipambana vikali kumaliza katika nafasi ya sita, kwani wakati mmoja alipokuwa mwisho, baada ya ajali kufanyika katika mashindano hayo.
Mpinzani wake mkali zaidi msimu huu, Fernando Alonso, wa timu ya Ferrari, alikamilisha mashindano akiwa katika nafasi ya pili, na hayo yakimaanisha Vettel alihitaji kumaliza katika nafasi sita za mwanzo ili kutangazwa bingwa.
Lakini mshindi wa mashindano hayo ya Formula 1 ya Brazil alikuwa ni Jenson Button, wa timu ya McLaren.
Button alimtangulia mwenzake wa timu ya Mclaren, Lewis Hamilton, aambaye gari lake liligongwa na dereva wa Force India, Nico Hulkenberg.
Mjerumani Hulkenberg alikuwa akijaribu kumpita Hamilton ili aweze kutangulia, na zikiwa zimesalia raundi 27, lakini hakuweza kulidhibiti gari lake vizuri, na liliteleza na kuligonga gari la Hamilton.
Hulkenberg aliadhibiwa, na kumaliza katika nafasi ya tano, nyuma ya mwenzake Alonso, Felipe Massa, aliyemaliza katika nafasi ya tatu, na dereva wa Red Bull, Mark Webber, akiwa katika nafasi ya nne.
Vettel, mwenye umri wa miaka 25, ndiye dereva mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya mashindano hayo kuweza kuandikisha ubingwa wa dunia mara tatu mfululizo.

Idhaa

No comments: