Siku
chache baada ya sakata la mwanamke anayedaiwa kufa na kufufukana, kisha
baadaye kuingia nyumbani kwake usiku akiwa mtupu, limechukua sura mpya
baada ya mwanamke huyo kuchukuliwa na mkuu wa wilaya ya Busega na
kumpeleka polisi.
Mkuu wa wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya,
alimchukua mwanamke huyo juzi na kumpeleka makao makuu ya polisi katika
mkoa wa Simiyu kwa usalama wake.
“Nimemchukua mwanamke huyo na kumpeleka
polisi kwa ajili ya usalama wake na kwa uchunguzi zaidi juu ya kisa
hicho...pia mwanamke anayetuhumiwa kuwa mchawi alichukuliwa na polisi
kwa ajili ya usalama wake sababu wananchi wenye hasira walitaka
kumshambulia,” alisema Mzindakaya.
Mwili wa marehemu huyo ulizikwa saa 12
jioni katika mji wa mwanamke anayedaiwa kumuua mwanamke huyo Ngulima
Kilinga (30), mkazi wa kitongoji cha Mwabulugu, kijiji cha Lamadi
wilayani Busega.
Awali wananchi walikuwa wamekataa kuuzika
mwili huo, kwa madai kuwa ni kitu kingine, ambapo mkuu huyo wa wilaya
aliingilia kati na kuwashawishi hao kuachana na imani za kishirikina.
Kabla ya kumchukua mwanamke huyo pia mkuu
huyo wa wilaya aliwahutubia wananchi, akiwaasa waachane na mambo ya
imani za kishirikina na kusisitiza kuwa huyo aliyekufa ndiye mhusika na
kwamba hakuna mtu aliyefufuka.
Alisema kuwa mwili wa mwanamke huyo
ulibadilika na kuwa kama sura ya mzee kutokana na kukaa kwa kipindi
kirefu bila kuwekwa kwenye jokofu, hali iliyosababisha tumbo kuvimba na
kutaka kupasuka.
“Nimewataka wananchi waachane na imani
hizo za ushirikina mimi ninaamini kwamba huyo mwanamke amekufa na wala
hajafufuka kama inavyodaiwa na watu wakiwemo ndugu zake...mwili wa
marehemu umebadilika kwa sababu haukuwekwa kwenye barafu,” alisema.
Kamanda wa polisi katika mkoa wa Simiyu, Salum Msangi, alikiri mwanamke huyo kufikishwa polisi.
Msangi alisema kuwa baada ya uchunguzi wa
kina kufanyika, imebainika kuwa mwanamke huyo anayedaiwa kuwa ndiye
aliyefufuka, ambaye mwili wake ulikuwa katika hospitali ya Mkula, si
kweli kwani anaonekana kuwa ana upungufu wa akili.
Alisema kuwa mwanamke huyo ametambuliwa kwa jina la Kundi Balekele (30), mkazi wa kijiji cha Mwasuguya wilayani Bariadi.
Kamanda Msangi alisema kuwa mwanamke huyo
alipotea nyumbani kwao kwa muda mrefu na kwamba huenda aliingia kwenye
nyumba ya marehemu huyo, katika kitongoji cha Mwabulugu kwa bahati mbaya
tu.
“Huyo mwanamke amekuwa akipotea mara kwa
mara nyumbani kwao na amepotea kwa muda mrefu, na pale nyumbani aliingia
kwa bahati mbaya maana ana upungufu wa akili,” alisema Msangi.
Alisema kuwa jana ndugu zake walifika kituoni hapo na kumchukua mwanamke huyo na kumpeleka kijijini kwao.
Aidha alifafanua kuwa kutokana na mwanamke
huyo kuingia kwenye nyumba hiyo usiku akiwa mtupu, na kuanza kuvaa nguo
za marehemu na kuangalia picha zake kwenye albamu, ikiwa ni pamoja na
kuita majina ya watoto wa marehemu na kisha kulala kitandani, ndiyo
sababu ndugu zake waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walidhani kuwa ndiye
ndugu yao kwani hata umbo la mwili wake ulifafanana na marehemu.
Alisema kuwa kwa kuwa mwanamke huyo ana
upungufu wa akili aliingia kwenye nyumba ya marehemu kwa bahati mbaya
akiwa mtupu, na hivyo kuwashangaza waliokuwa ndani ya nyumba hiyo na
kudhania kuwa ndugu yao amefufuka, kutokana na matendo aliyokuwa
anafanya akiwa ndani ya nyumba hiyo.
Kwa upande wao ndugu wa marehemu akiwemo
mama yake mzazi, Mwashi Myeya, alisema kuwa mwanamke aliyechukuliwa na
mkuu wa wilaya ndiye mtoto wake kwani ana alama usoni ambayo alikuwa
nayo kuanzia utotoni na kwamba hayo ni mazingara yamefanyika.
“Siwezi kumsahau mwanangu nimemuona anayo
alama kwenye sehemu ya pua na hiyo alama ni kutoka utotoni alikuwa
nayo,” alisema Myeya.
Wananchi hao walisema kuwa mwili wa
marehemu waliouzika ni kitu kingine na ndio maana waliamua kuuzika
kwenye mji wa mtuhumiwa wa uchawi, ambaye pia alitoroshwa na polisi kwa
ajili ya usalama wake.
Aidha, wanadugu hao walisema kuwa iwapo
mwanamke huyo asingetoroshwa na polisi, huenda angefanya dawa za
kumtengeneza na kurudia hali yake.
Hata hivyo kabla ya mkuu wa wilaya
kumchukua mwanamke huyo, aliletwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya
kumtengeneza ili arudie hali yake, ambapo alidai apewe kiasi cha Sh.
milioni 2.5 ambapo wananchi walianza kuchanga lakini pia hazikutimia.
Habari zinasema kuwa baada ya mkuu wa
wilaya kufika katika eneo la tukio mganga huyo alitoweka katika eneo
hilo katika mazingira ya kutatanisha na kutokomea kusiko julikana.
Imeelezwa kuwa mwanamke huyo alifariki
dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Mkula
inayomilikiwa na kanisa la AIC, ambapo mwili wake ulihifadhiwa chumba
cha maiti.
Mashuhuda walisema kuwa saa 7 usiku
mwanamke mmoja aliyekuwa mtupu alingia ndani ya nyumba ya marehemu na
kuanza kuita watoto wake, ikiwa ni pamoja na kuvaa nguo za marehemu,
ambapo ndugu zake walidhani kuwa amefufuka.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment