Sakata
la mfungwa aliyekutwa uraiani akiwa na bunduki na risasi, limeingia
katika hatua mpya baada ya Jeshi la Polisi na Magereza kutoa kauli
zinazokinzana.
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu limeendelea
kuthibitisha kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa nyumbani kwake Novemba 16,
mwaka huu akiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), risasi 31 na
magazini tatu, Masanja Maguzu (42), ni mfungwa ambaye hajamaliza
kutumikia kifungo cha miaka 15 jela na kuwa alitoka gerezani katika
mazingira ya kutatanisha.
Wakati Jeshi la polisi likisisitiza hivyo, Jeshi la Magereza limetoa taarifa inayoeleza kuwa mtu huyo alishamaliza kifungo.
Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Salum
Msangi, amekanusha madai ya Jeshi la Magereza kwamba mfungwa huyo
alishamaliza kutumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka mitano jela na
kwamba hata kama alikuwa akitumikia adhabu ya miaka mitano muda huo bado
haujatimia.
Kamanda huyo alifafanua jana kuwa hata
kama kuna tetesi za mfungwa huyo kuachiwa kwa msamaha wa Rais, makosa
yaliyompeleka gerezani kwa mujibu wa Sheria ya Msamaha hayana msamaha.
Alisema mfungwa huyo alihukumiwa kifungo
cha miaka 15 jela mwaka 2010 baada ya yeye na mwenzake, Japhet
Sylivester, kupatikana na hatia ya kukamatwa na SMG, risasi 622 na nyara
za serikali (nyama ya nyati) akiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti (Senapa).
Kamanda Msangi aliiambia NIPASHE kwa njia
ya simu kuwa leo atatoa taarifa kamili ya jinsi mfungwa huyo alivyotoka
gerezani baada ya Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kubaini
ukweli wa mazingira yaliyosababisha kuwa uraiani.
Alifafanua kuwa wafungwa hao walikuwa
wakiitumia bunduki hiyo kufanyia vitendo vya uhalifu ukiwamo ujambazi na
ujangili na siku hiyo walikamatwa nayo ndani ya hifadhi hiyo na risasi
74 na baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi na wa wanyamapori aliwapeleka
nyumbani kwake kuwaonyesha alipokuwa ameficha nyingine 548.
Alidai kuwa wafungwa hao walikamatwa
katika msako wa pamoja wa kukabiliana na vitendo vya uhalifu na
kukabiliana na ujangili uliokuwa ukiendeshwa kwa pamoja kati ya askari
wa Jeshi la Polisi na Wanyamapori mkoani Shinyanga kwa wakati huo.
Alisema baada ya kufunguliwa mashitaka
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Shinyanga, watuhumiwa hao
walipatikana na hatia na hivyo kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 15
jela kila mmoja.
“Kesho (leo), nitatoa picha kamili ya
jinsi mfungwa huyo alivyotoroka gerezani na kumuacha mwenzake
waliyehukumiwa naye kifungo, hii ni baada ya kufanya uchunguzi wetu wa
kina na kumhoji mfungwa mwenyewe na kubaini mambo kadha wa kadha
yaliyosababisha yeye kuwa uraiani na kuendelea kufanya vitendo vya
uhalifu na ujangili kwa kutumia silaha za kivita,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, wafungwa hao
walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi ambayo ni
kupatikana na bunduki, risasi, nyara za serikali na kuingia na kuwinda
ndani ya hifadhi bila kibali na baada ya kupatikana na hatia na
kuhukumiwa kwenda gerezani, hayawezi kutolewa msamaha.
“Watuhumiwa hawa walipatikana na makosa ya
kupatikana na bunduki ya kivita, kupatikana na risasi, kupatikana na
nyara za serikali na kuingia kuwinda ndani ya hifadhi na kuwinda bila
kibali nyume cha sheria makosa yote haya yanaangukia kwenye makosa ya
uhujumu uchumi ambayo hayana msamaha kisheria,” aliongeza.
Alisema siku 10 kabla ya kumkamata mfungwa
huyo akiwa uraiani na SMG hiyo, risasi 31 na magazini tatu, moja
hutumika katika bunduki aina ya Uzi gun ya Kiisraeli, jeshi hilo
lilikuwa limemkamata mke wake, Holo Mabuga (30), akiwa na bunduki ya
kivita aina ya G3, risasi zake 36 pamoja na risasi nyingine zinazotumika
kwenye bunduki aina ya SMG inayodaiwa pia kutumika katika matukio
mbalimbali ya kihalifu na ujangili katika Senapa na Pori la Akiba la
Maswa.
TAARIFA YA MAGEREZA
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari
na kusainiwa na Kaimu Kamishna wa Magereza, Deonice Chamulesile, ilisema
Maguzu alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano, lakini Aprili 26,
mwaka huu alikuwa ameachiliwa.
“Mfungwa aliyekuwa na Namba 250/2010,
Masanja Maguzu, alipokelewa Gereza la Wilaya ya Shinyanga tarehe 3
Novemba, 2010 baada ya kuhukumiwa na Mahakama ya wilaya hiyo kwa makosa
mbalimbali ya uhujumu uchumi,” alisema.
Aliongeza: “Alianza kutumikia kifungo cha
miaka mitano gerezani kuanzia Novemba 3, 2010 na kufikia Aprili 26,
2012 aliachiliwa baada ya kutimiza masharti ya kifungo na kutoka
gerezani kwa mujibu wa sheria, hivyo ifahamike kwamba hakutoka katika
mazingira ya utata kama ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari.”
Taarifa hiyo iliyataja makosa
aliyohukumiwa kuwa ni kuingia kinyume cha sheria katika hifadhi, kuwinda
kunyume cha sheria na kumiliki kinyume cha sheria nyara za serikali.
Taarifa hiyo ya Chamulesile ilieleza kuwa
katika kosa la kwanza, Maguzu alihukumiwa miaka miwili jela, kosa la
pili miaka mitano jela na la tatu miaka mitano jela.
Alisema hukumu iliyotolewa iliamuru adhabu hizo zitumikiwe kwa pamoja kwa kufungwa miaka mitano jela.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment