Friday, April 26, 2013

UN kupigia kura azimio kuhusu Mali


Baadhi ya wanjeshi wa Chad walio nchini humo pia wataanza kundoka
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupigia kura azimio linalopendekeza kuundwa kwa kikosi cha kulinda amani nchini Mali.
Kikosi hicho chenye wanajeshi 12,600 kinajumuisha takriban wanajeshi 6,000 kutoka nchi za Magharibi mwa Afrika ambazo tayari zina wanajeshi wao nchini humo.
Azimio hilo limependekezwa na Ufaransa ambayo iliingilia kati mzozo wa Mali mnamo mwezi Januari ili kupambana na wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini mwa nchi hiyo.
Kikosi hicho kinatarajiwa kwenda Mali mwanzoni mwa mwezi Julai kabla ya uchaguzi mkuu.

Hata hivyo duru zinasema kuwa azimio hilo limezua mjadala mkali.

Makundi ya kiisilamu yaliweza kutumia pengo la usalama lililotokea baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka jana na kuanza kushinikiza watu kufuata sheria za kiisilamu.
Miji iliyo Kaskazini mwa nchi, imeweza kudhibitiwa na jeshi la Ufaransa lakini baadhi ya wapiganaji wangali katika maficho yao.
Ufaransa ilianza kuondoa baadhi ya wanajeshi wake 4,000 mapema mwezi huu kutoka nchini humo, lakini imekuwa ikishinikiza Umoja wa Mataifa kupeleka wanajeshi wake.
Aidha wanajeshi wa Chad, wanasemekana kuwa wenye uzoefu mkubwa zaidi katika kupambana na wapiganaji jangwani, lakini nchi hiyo pia imeanza kuondoa wanajeshi wake kutoka Mali.
Sababu ya kikosi cha Umoja wa mataifa ni kulinda amani na kitakuwa na wanajeshi 11,200, pamoja na polisi 1,440.
Lengo lake kuu litakuwa kuweka uthibiti katika baadhi ya sehemu za Kaskazini mwa Mali ili kumaliza vitisho kutoka kwa wapiganaji wa kiisilamu.
Hata hivyo rasimu ya azimio hilo haisemi ikiwa wanajeshi hao wataweza kupigana na wapiganaji wa kiisilamu wenye uhusiano na kundi la al-Qaeda, lakini wanajeshi 1,000 wa Ufaransa,wataweza kusalia Mali.

No comments: