Tegemea picha zaidi za ‘asset’ ya Agnes Gerald aka Masogange kwenye Instagram sababu video vixen huyo ni mtu huru kabisa.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la
leo, Mahakama ya Kempton ya jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini
imemwachia huru mrembo huyo baada ya kulipa faini ya R30,000 ambazo ni
sawa na shilingi milioni 4.8 za Tanzania, kubeba kemikali zinazotumika
kutengeneza dawa za kulevya.
Naye Melissa Edward ameachiwa huru na mahakama hiyo, baada ya kukosekana ushahidi wowote wa kumtia hatiani.
Habari hiyo kwenye gazeti la Mwananchi inaeleza kwa urefu:
Msemaji wa Kitengo cha Uchunguzi wa
Makosa ya Jinai cha Afrika Kusini(Hawk), Kapteni Paul Ramaloko alisema
Watanzania hao wameachiwa huru baada ya kuonekana kuwa hawakubeba dawa
za kulevya, bali kemikali aina ya ephedrine.
Mahakama hiyo ilibaini kuwa, Melissa
hana hatia kwa kuwa ilionekana kuwa amemsindikiza Masogange, ambaye
alimwomba amsaidie kubeba mzigo huo.
“Mahakama iliona kuwa Melissa aliombwa
tu kumsaidia kubeba baadhi ya mabegi, lakini hayakuwa yake. Mizigo yote
iliandikwa jina la Agness Gerald na si Melissa,” gazeti la Mwananchi
limemnukuu Kapteni Ramaloko.
Alisema, Melissa alijitetea kuwa hakuwa
amesafiri pamoja na Masogange bali walikutana ndani ya ndege na
Masogange alimwomba amsaidie kubeba mizigo hiyo, kwani ilikuwa mikubwa.
Kwa sheria za Afrika Kusini kubeba
kemikali zozote ambazo zimepigwa marufuku ni kosa la jinai kisheria,
hivyo mahakama iliamuru Masogange ahukumiwe kwenda jela kwa miezi 30
(miaka miwili na miezi mitano) au alipe faini ya R30, 000 (sawa na Sh4.8
milioni).
Hata hivyo, Kapteni Ramaloko alisema mdhamini wa Masogange alilipa nusu ya fedha na kwamba zinazobaki amalizie baadaye.
Alisema kutokana na kutomalizia kulipa
fedha hizo ataendelea kubaki nchini humo hadi atakapomaliza kulipa nusu
ya faini iliyobaki.
Masogange na mwenzake walipokamatwa na SARS ilielezwa walikuwa wamebeba dawa za kulevya aina ya
Methamphetamine, lakini Mahakama juzi ilithibitisha walikamatwa na kemikali aina ya Ephedrine, ambayo siyo dawa za kulevya.
Wakati Kamishna Mkuu wa Kitengo cha
Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Geofrey Nzowa alipoulizwa na Mwananchi
Jumamosi juzi alisema mzigo walioubeba Masogange na mwenzake haukuwa ni
dawa za kulevya bali ni kemikali za dawa za kulevya, lakini Msemaji wa
Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini, (SARS), Marika Muller alieleza kuwa
timu ya SARS ina uhakika kuwa mabegi sita yaliyokamatwa Julai 5 ni dawa
za kulevya aina ya Methamphetamine.
Jana, Muller alipoambiwa kuwa Watanzania
hao wameachiwa huru baada ya kulipa faini na mmoja kuachiwa huru kwa
kuwa Mahakama imeridhika kuwa hazikuwa methamphetamine bali kemikali
aina ya Ephedrine, alirudia tena na kueleza kuwa, mamlaka hiyo ina
uhakika na kazi yake na iwapo mahakama imewaachia huru basi yeye hana la
kusema zaidi.
“Kazi yetu kubwa ni kukamata mizigo
haramu inayopitishwa uwanja wa ndege, kama Mahakama imeona kuwa si dawa
za kulevya, hatuna la kuongeza. Kikubwa tumemaliza kazi yetu,” alisema
Muller kwa kujiamini.
Hata hivyo, Nzowa jana akizungumzia
kuachiwa huru kwa Watanzania hao, alionyesha kushangazwa jinsi Mahakama
ilivyotoa adhabu ndogo.
“Hii ni ajabu sana. Kama watu wamebeba
mzigo wenye thamani ya Sh6.8 bilioni wanapigwa faini ya milioni nne,
hawataogopa kufanya hiyo biashara. Hao watu ni hatari sana,” alisema
Nzowa.
Alipoulizwa iwapo wakirudi Tanzania
wanaweza kushtakiwa, Nzowa alisema kitengo chake hakitaweza kuwashtaki
tena kwa sababu wanaweza kujitetea kuwa tayari walishahukumiwa,
isipokuwa Mwendesha Mashtaka aliyekuwa akisimamia kesi yao anaweza
kukata rufaa.
“Iwapo Mwendesha Mashtaka wa huko
akikata rufaa kwa kuona adhabu aliyopewa mhalifu huyo ni ndogo, anaweza
kufanya hivyo,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema, inasikitisha kuwa wakati mapambano ya biashara hiyo yakiwa yanaendelea Tanzania, watuhumiwa hao wanaachiwa.
“Adhabu waliyopewa ni ndogo hasa wakati
huu ambao Tanzania tunachafuka kwa tuhuma hizi. Lazima kitu kifanyike
kubadili hali halisi hapa nchini,” alisema.
Nzowa alieleza kuwa alikwenda Afrika
Kusini tangu Septemba Mosi kuwahoji wasichana hao ambao hata hivyo
hawakuweza kusema lolote la kuisaidia polisi.
Masogange aliandika kwa maandishi kuwa
ni kweli mzigo ulikuwa wa kwake, lakini akasema mdogo wake, ambaye ni
Melissa, hajui lolote na alikuwa amemsaidia.
Julai 5, mwaka huu Masogange na Melissa
walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo
wakidaiwa wamebeba kilo 150 zilizodaiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya
Methamphetamine zenye thamani ya Sh6.8 bilioni.
Dawa hizo zilizokuwa zimepakiwa katika
mabegi makubwa sita, zinatajwa kuwa ni kiwango kikubwa kukamatwa katika
historia ya SARS ndani ya uwanja huo unaotumiwa na mataifa makubwa
duniani.
Taarifa za kukamatwa kwa wasichana hao
zilipamba kurasa mbalimbali za magazeti ndani na nje ya Tanzania, jambo
lililosababisha Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kuchukua hatua
za kuusafisha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
Baada ya uchunguzi wa Dk Mwakyembe ambao
ulibaini kuwapo mchezo mzima uliochezwa wakati Masogange na Melissa
walipokuwa uwanja wa ndege.
Agosti 17 alitoa agizo la kufukuzwa
kazi, Koplo Juliana Thadei, Jackson Manyoni, Yusuph Daniel Issa, Koplo
Ernest na Mohamed Kalugwan.
Mwakyembe alisema katika hali isiyokuwa
ya kawaida mfanyabiashara ambaye hakuwa na tiketi ya kusafiri siku hiyo,
baadaye alibadili mawazo hapohapo na kuamua kuondoka siku hiyo kwenda
Afrika Kusini na kulipia faini ya dola 60 (Sh96, 000) ili kupata tiketi.
Pia Mwakyembe aliliagiza Jeshi la Polisi
kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kumkamata mfanyabiashara
anayedaiwa kumsaidia Masogange kusafirisha dawa za kulevya ambaye
alitoweka na mabegi matatu ya dawa hizo huko Afrika Kusini.
Source: Mwananchi