Mmoja wa waasi wa
Sudan anayeshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kwa makosa
ya uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur ameuawa, kwa mujibu wa jopo
la mawakili wake wa utetezi.
Taarifa zinasema, Saleh Mohammed Jerbo Jamus alifariki dunia Ijumaa iliyopita mchana wakati wa mapigano huko Darfur Kaskazini.Mwandishi wa BBC mjini The Hague, Uholanzi anasema lazima mahakama hiyo ipate uthibitisho kuhusu kifo hicho kabla ya kuifuta kesi.
Jerbo na kiongozi mwenzake wa waasi wa Darfur, Abdallah Banda Abakaer Nourain wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uhalifu wa kivita yanayohusishwa na mauaji ya askari 12 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika katika shambulio lililofanyika katika kambi ya askari hao ya Haskanita Septemba 2007.
Jerbo aliuawa wakati wa shambulio kwenye makazi yake lililofanywa na wapiganaji wa kundi lililojitenga kutoka kundi la Justice and Equality Movement linaloongozwa na Gibril Ibrahim.
Watu hao wawili walijisalimisha kwa hiari katika mahakama ya ICC mwaka 2010 ili kukabili mashtaka, na walikua huru kuondoka Uholanzi na kurudi mahakamani pale walipohitajika.
Kwa mujibu wa ICC, Jerbo alikuwa ni Mnadhimu Mkuu wa kundi la waasi la SLA – Unity, wakati wa shambulio la mwaka 2007, lakini sasa alikuwa kwenye kundi la Justice and Equality Movement.
Rais wa Sudan, Hassan Omar Al Bashir, mawaziri wake wawili na kiongozi mmoja wa kundi la wanamgambo linaloiunga mkono serikali pia wameshtakiwa na mahakama ya ICC kwa uhalifu wa kivita Darfur lakini mpaka sasa hawajakamatwa.
Wote wamekanusha mashtaka dhidi yao wakidai kwamba, machafuko ya Darfur yametiwa chumvi kwa sababu za kisiasa.
Mzozo wa Darfur ulianza miaka 10 iliyopita baada ya waasi kuanza kushambulia maeneo ya serikali, wakiishutumu Khartoum kwa kuwakandamiza Waafrika na kuipendelea jamii ya Kiarabu.
Kundi la wanamgambo wa Kiarabu la Janjaweed, wakati huo lilishutumiwa kwa kuendesha mauaji ya kikabila dhidi ya raia Waafrika wa Darfur.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu 300,000 walipoteza maisha kutokana na mzozo wa Darfur. Lakini serikali ya Khartoum inaweka idadi hiyo kuwa ni watu 12,000.
Watu wengine zaidi ya milioni 1.4 wameachwa bila makaazi. Ingawa machafuko ya Darfur yamepungua sana bado kuna mapigano kati ya vikosi vya serikali, waasi, na vikundi vinavyotofautiana kikabila.