Tuesday, December 18, 2012

Tanesco iwe wazi kwa kutangaza mgawo rasmi

Maoni ya Katuni
Katika  toleo letu  la jana, tulichapisha habari ndefu kuhusiana na malalamiko ya watumiaji wa umeme nchini kukatiwa umeme kila wakati bila Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoa taarifa.

Uchunguzi wa gazeti hili  katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na ujumbe mfupi wa simu za mikononi (sms) uliotumwa na watumiaji wengi wa umeme, vimebainisha kuwa kuna tatizo kubwa kutokana na Tanesco kukata umeme bila kutoa taarifa kwa wateja wake  kuhusiana na sababu zinazosababisha hali hiyo.

Wateja wa shirika hilo walieleza kwa uchungu kuwa kutokana na kukatiwa umeme bila taarifa wamekuwa wakijikuta wakipata hasara kutokana kuungua kwa  vifaa vyao vinavyotumia umeme kama majokofu, pasi, redio na televisheni.

Wateja hao wanaeleza kuwa hali hiyo imekuwa inatokana na umeme kurudishwa ghafla bila vifaa hivyo kuzimwa.

Mbali na kuungua kwa vifaa vya  watumiaji wa umeme, ukataji wa umeme bila taarifa umewasababishia hasara wafanyabiashara wakubwa wenye viwanda pamoja na wachuuzi kutokana na kukaa muda mrefu bila kufanya shughuli zao.


Kwa mfano, kuna wazalishaji ambao kama wangefahamu kuwa kuna mgawo wangejiandaa kwa kununua majenereta makubwa badala ya kusubiri umeme urudi pale unapokatika.

Vile vile, wauzaji wa vinywaji baridi, vinyozi, watengenezaji nywele wanawake na wajasiriamali wengine wamejikuta wakikwama kutokana na shughuli zao kusimama tena bila kujua lini umeme utarejeshwa kutokana na kutokuwepo kwa ratiba.

Inawezekana kama Tanesco wangekuwa wawazi kwa kueleza umma kuwa kuna matatizo yanayosababisha kuwepo kwa mgawo, pengine baadhi ya watumiaji wangeweza kujiandaa vizuri kwa lengo la kuendelea na shughuli zao.

Lakini ukimya wa Tanesco unawafanya baadhi ya watumiaji kuamini kuwa hakuna tatizo kubwa la kuwalazimisha kuchukua hatua mbadala, kwa maneno mengine kutafuta aina nyingine ya nishati.

Kwa ujumla malalamiko yao yalikuwa ya kusikitisha kutokana na hasara ambayo imewapata  baadhi yao kutokana na Tanesco kutokuwa wawazi katika kuwahudumia wateja wake.

Mara nyingi watumiaji wamekuwa wakilalamikia kukatiwa umeme kwa muda mrefu bila shirika hilo kutoa taarifa, lakini mara zote viongozi wake wamekuwa wakitoa matamko na kauli za kukanusha.

Kauli za siku zote za watendaji wa Tanesco na viongozi wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini ni kwamba hakuna mgawo bali shirika linafanya marekebisho ya miundombinu ikiwamo kuhamisha nguzo na nyingine zinazofanana na hizo.

Kufuatia uchunguzi wetu na malalamiko ya wateja, Tanesco limekanusha kuwapo kwa mgawo wa umeme nchini na kusema kuwa ni hitilafu za kiufundi zinazojitokeza.

Shirika hilo limesema kukatika kwa umeme kunatokana na matatizo ya kiufundi kama kukatika kwa nyaya za umeme, kuanguka kwa nguzo za umeme pamoja na kuharibika kwa vifaa kwenye transfoma.

Kwa mujibu wa Tanesco, matatizo mengine ni kuibwa kwa mafuta ya transfoma, urekebishwaji waa mifumo ya umeme, feeder kupata matatizo, kuharibika kwa Droper Out fuse, Optic fiber, Feeder za Nodick na Jamper za Nodick kukatika.

Tunalishauri shirika hilo kuchukua hatua kwa kuutangazia umma kwamba kuna mgawo wa umeme badala ya kutoa kauli ambazo zinawakwaza wateja badala ya kuwasaidia.

Kuwatangazia kuwa kuna mgawo kutokana na sababu zilizoainishwa hapo juu kutasaidia watumiaji wa umeme kujiandaa kukabiliana na matatizo hayo.

Kwa bahati mbaya sana, katika miaka ya karibuni, suala la umeme limegeuzwa la kisiasa zaidi kuliko hali halisi.

Baadhi ya watendaji na wanasiasa hawataki kueleza kuwa kuna matatizo katika sekta ya umeme, badala yake wanapenda kutoa kauli na matamko ya kuwapa wananchi matumaini yasiyokuwepo.

Wengi tunaelewa kuwa nchi yetu inakabiliwa na tatizo kubwa la nishati ya umeme hivyo Tanesco iwajibike kwa kuwatangazia watumiaji na wananchi kwa ujumla kuwa kuna mgawo wa umeme.
CHANZO: NIPASHE

No comments: