Tuesday, December 18, 2012

Siri yafichuka mauaji Polisi

  *Askari mwenzao aanika kilichotokea
Mkuu wa Polisi nchini, Said Mwema
Mapya yameendelea kuibuka kufuatia madai kuwa vifo vya watu watatu wakiwamo polisi wawili wilayani hapa vimetokana na askari hao kukusanya kwa nguvu mapato ya serikali.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zimedai kuwa askari hao wa Kikosi cha Usalama Barabarani, walikwenda katika kijiji na kata ya Mugoma kukamata vyombo vya usafiri na watu wanaoendesha bila leseni ili kuhakikisha wanafikisha kiwango cha makusanyo ya serikali waliyopangiwa kila mwezi.

Chanzo chetu kimeeleza kuwa Askari wa Usalama Barabarani wanapaswa kukusanya kiasi kisichopungua Shilingi milioni tatu kila mwezi na hatua hiyo imekuwa ikiwalazimu kwenda kukamata na kutoza faini mbalimbali katika maeneo hata yasiyo na usalama kwa maisha yao.

Kikizungumzia tukio la mauaji hayo, chanzo hicho kilidai kuwa kitendo cha polisi kwenda kukamata pikipiki iliyokuwa ikitengenezwa na mtuhumiwa huyo ambaye ni fundi jirani na gulio la kijiji hicho, hakikuzingatia taratibu.

Kwa msingi huo, chanzo hicho kimeeleza kwamba Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani ndiye anayepaswa kuwa mlalamikiwa wa kwanza katika mauaji hayo.

“Unajua ndugu mwandishi, haiwezekani kwenda kukamata pikipiki za watu hadi ndani ya gulio...mbaya zaidi unakwenda kukamata na pikipiki inayotengenezwa kwa fundi. Hakika hapa busara haikutumika hata kidogo, ndiyo maana mauaji kama haya yametokea,” kilidai chanzo hicho na kuongeza:

“Pamoja na kwamba Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuwa mlalamikiwa wa kwanza, kwa kiasi kikubwa serikali yetu nayo inachangia maana sisi askari wa usalama barabarani tunalazimika kuhakikisha tunafikisha kiwango cha fedha tunazopangiwa kwa kila mwezi na inapotokea tarehe zinaelekea ukingoni na makusanyo hayajafikia, matokeo yake ndiyo hayo.”

Chanzo hicho kilipingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, kwamba askari hao walikuwa kwenye operesheni maalum ya kukamata watu wasio na leseni na vyombo vya moto visivyofaa kwa matumizi ya usafirishaji wa abiria.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, taarifa hiyo imechakachuliwa kwa lengo la kukwepesha ukweli wa jambo hilo kujulikana.

“Hakika hapakuwa na operesheni maalum kama Kamanda alivyodai isipokuwa ni utaratibu wetu wa kawaida kwenda kukusanya mapato ya serikali. Tatizo hapa ni kutaka kukwepesha ukweli wa mambo. Aidha, yeye mwenyewe au mkuu wa upelelezi wa wilaya ambaye atakuwa ameamua kuchakachua maelezo ili kuweka kinga ya kuonekana askari walikuwa kwenye makosa,” kilidai chanzo hicho.

Hata hivyo, Kamanda Kalangi alipoulizwa jana kuhusiana na taarifa hiyo, alisisitiza kuwa ilikuwa operesheni.

“Mimi ndiye Kamanda, kama kuna anyepinga taarifa nilizozitoa kamuulize huyo huyo,” alisema Kamanda Kalangi.

Alisema kutokana na mauaji hayo, Mkuu wa Polisi nchini, Said Mwema, ametuma kikosi maalum kutoka makao makuu ya polisi kinachotarajiwa kuingia mkoani Kagera jana. Hata hivyo, hadi jioni hakikuwa kimewasili.

Alisema kikosi hicho kitaungana na wenzao wa mkoani Kagera kuchunguza kwa kina mauaji hayo askari hao wawili pamoja na raia mmoja.

WATU 11 WASHIKILIWA

Kadhalika, Kamanda Kalangi alisema mpaka juzi  usiku, watu 40 walikuwa wametiwa mbaroni kufuatia msako mkali wenye lengo la kuwabaini waliohusika na mauaji hayo.

Bila kuwataja majina yao, alisema baada ya kufanyika upelelezi kwa watu hao, wengine 29 waliachiwa huru huku 11 wakiendelea kuchunguzwa.

Kamanda Kalangi alisema idadi ya watuhumiwa hao inaweza kupungua au kuongezeka zaidi kwa kuwa upelelezi bado unaendelea.

Polisi waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Koplo Paschal na Konstebo Alexander na raia ni Said Mkonikoni (24), aliyekuwa mkazi wa Kata ya Mugoma.

Katika tukio hilo ambalo wananchi walilazimika kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaua polisi wawili, pia waliteketeza kwa kukichoma moto Kituo cha Polisi cha Mugoma na kusababisha nyaraka za serikali, pikipiki, baiskeli na silaha kuungulia ndani.

Hata hivyo, thamani ya  uharibifu huo bado haijafahamika mpaka sasa.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na NIPASHE walidai kuwa hawana amani kutokana na kamata kamata inayoendelea kufanywa na polisi na kusababisha baadhi yao kushindwa kwenda kufanya shughuli za uzalishaji mali wakihofia kutiwa nguvuni.

Hali hiyo imedaiwa kusababisha baadhi ya wananchi kugeuka wakimbizi baada ya kuvuka mpaka na kuingia nchini Burundi kukwepa kukamtwa na polisi wanaoendesha msako katika maeneo mbalimbali ya wilayani humu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: