Friday, November 29, 2013

BERKO KULIPWA MSHAHARA MKUBWA KULIKO KASEJA






Kipa wa zamani wa Yanga, Yaw Berko anatua nchini leo akitokea kwao Ghana akiwa kipa ghali zaidi kwa kuwa atalipwa mshahara mkubwa hata kuliko Juma Kaseja wa Yanga.

Berko anatua nchini saa nne asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na mara moja atakwenda kumalizia mazungumzo na Simba na tayari wamekubaliana mshahara wake utakuwa dola 1,500 (Sh 2,400,000), kwa mwezi.
Mabingwa Yanga wanamlipa Kaseja aliyekuwa ameachwa na Simba Sh milioni 2, sawa na mshambuliaji mwingine wa Yanga, Mrisho Ngassa ambaye pia aliichezea Simba msimu uliopita.
Lakini katika mazungumzo yake, kipa huyo ameutaka uongozi wa Simba kumhakikishia kwamba kipa Abel Dhaira raia wa Uganda anabeba virago vyake na kuondoka.
“Berko amesema yuko tayari kuja nchini na kuanza kazi lakini asingependa hata kidogo kuona Dhaira yupo. Ndiyo kilikuwa kitu cha kwanza ambacho hakihitaji kukiona na kweli tumefanya hivyo kwa kuwa hata Dhaira mwenyewe ameonyesha anataka kuondoka,” kilieleza chanzo kutoka ndani ya Simba.
Hata hivyo, Simba italazimika kumsajili kwa nusu msimu tu kwa kuwa TFF tayari imetangaza kuanzia msimu ujao, imepitisha sheria ya timu kutosajili makipa wa kigeni.
Berko aliondoka nchini Yanga ikiwa inamhitaji, lakini ililazimika kumtumia Ally Mustapha ‘Barthez’ aliyekuwa kipa wa pili baada ya kipa huyo kuonyesha usumbufu na maringo huku viongozi wakilalamika alikuwa si mtu anayejituma.